Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amewataka watanzania kuondoa hofu juu ya dawa za asili zinazozalishwa nchini na badala yake wazitumie kwani zina msaada mkubwa katika kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwamo yale ya upumuaji.
Aliyasema hayo juzi wakati alipotembelea shirika la utafiti na Maendeleo ya viwanda (Tirdo) ambao walizindua rasmi dawa aina ya Covidol inayoaminika kukinga maambukizi ya magonjwa mbalimbali.
“Tunatumia miti shamba yetu lakini pia tunatumia utaalamu kutengeneza dawa hizi na zinapita kwenye vipimo maabara zinachekiwa kwahiyo niwaambie tutumie dawa hizi tukiwa tuna uhakika ni dawa nzuri, zimetengenezwa kitaalamu, na hazina madhara,” alisema Kunenge.
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya Rais wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kuwataka watanzania kutumia dawa za asili katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona (Covid-19).
Februari 4 mwaka huu akija Dodoma Rais Magufuli alisisitiza juu ya matumizi ya miti shamba pamoja na kujifukiza kama njia za kupambana na Covid-19 akisema kuwa si kila dawa zinazotoka nje ya nchi ni nzuri kwa watanzania.
“Kuna dawa inaitwa Covidol, Bugiji zinafanya kazi kwasababu zimekuwa proved na mkemia mkuu, kamwe msifikirie kila dawa inayotoka nje ni kwaajili yenu, ingekuwa hivyo malaria ingeisha….,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa kiwandani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Dar, Kunenge alilipongeza Tirdo kwa jitihada kubwa za kuendeleza viwanda vya ndani hasa kwenye tafiti na uvumbuzi wa dawa mbalimbali za asilia.
“Niwashukuru kwa mchango mkubwa mnaofanya katika maedeleo ya viwanda katika nchi yetu, mkoa wetu wa Dar es Salaam ni mkoa wa kibiashara na tunataka kuhakikisha tunaweka mazingira bora zaidi ya biashara ambapo itatusaidia kuongeza viwanda vitakavyosaidia kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na ajira za kutosha,” alisema Kunenge.
Mgunduzi wa dawa hiyo Profesa Malebo Khamis alisema kwa kutumia tafiti wameweza kuvumbua dawa hiyo yenye uwezo wa kupambana na matatizo ya upumuaji ambapo mpaka sasa chupa 50,000 zinazalishwa kwa siku.
“Ujumbe wangu ni mmoja tu kwamba tunayo dawa inayofanya kazi, inayokinga na inayoponya,” alisema mgunduzi huyo.
Post A Comment: