Mratibu wa mradi wa kutokomeza ukatili na ukeketaji kutoka Shirika la la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), Annamaria Mashaka akitoa mafunzo mbele ya watu maarufu na Mangariba wastaafu, mafunzo yaliyofanyika jana katika Shule ya Sekondari Mungumaji.
Mmoja wa watoa elimu kutoka Shirika la ESTL, Brigita Mwaka akitoa mafunzo kwa Vijana wa Mungumaji walio nje ya Shule..
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL)Mkoa wa Singida limekutana na makundi mbalimbali ya wakazi wa Kata ya Mungumaji kujadili namna ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Katika kuhakikisha ukatili wa Kijinsia unaisha, Shirika hilo limeandaa mpango kazi katika Mradi wake wa mwaka mmoja wa Kutokomeza ukatili na ukeketaji mkoani hapa Mradi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Finland nchini.
Mratibu wa Mradi huo Bi Annamaria Mashaka kutoka Shirika hilo la (ESTL) alisema katika jitihada za kutokomeza ukatili Shirika limelenga kuyafikia makundi mbalimbali ya wananchi wa Mkoa wa Singida ambayo ni Wanawake, Watoto wanaosoma shule za Msingi,Vijana walio nje ya Shule,Wakunga wa Jadi pamoja na watu maarufu.
Makundi mengine ambayo Shirika limelenga kuyafikia ni Mangariba wastaafu,Wahudumu wa afya ngazi ya jamii,Kamati za ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ngazi zote pamoja na Viongozi wa Dini,na lengo ni kuongeza uelewa,kubadili mtazamo,mabadiliko ya tabia dhidi ya ukeketaji na mifumo ya aina mbalimbali za ukatili dhidi ya Watoto, Wasichana na Wanawake.
"Tumelenga kuyafikia makundi haya ili tuwape Elimu ya namna ya kutokomeza ukatili kwasababu haya makundi yanafikika moja kwa moja kwenye jamii hivyo wakipata hii Elimu tunaamini jamii itaelimika." alisema Annamaria.
Alisema mpaka sasa tayari wameyafikia makundi hayo katika Kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Singida kutoa Elimu hiyo ambapo pia zoezi hilo linaendelea katika Manispaa ya Singida kwenye kata za Mungumaji,Kisaki,Unyambwa na Uhamaka.
Kwa upande wao Viongozi wa Dini katika mafunzo yao walishauru na kuhimizana kwenda kuwafundisha waumini wao masuala ya mahusiano na kubainisha athari zake kuliko kuogopa na kuficha ile hali Watoto wanajifunza kwenye Television na sehemu zingine ambazo wakati mwingine hazionyeshi athari zake,hivyo kupelekea Watoto kujiingiza kwenye ndoa za utotoni na mambo mengine.
Huku Katibu wa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Mungumaji Juma Athuman akifikirisha Viongozi wa Dini hiyo kuangalia namna ya kubadilisha muda wa madarasa ya Watoto wanajifunza Madrisa saa za jioni kwani inapelekea Watoto hao kuingia kwenye vishawishi.
Washiriki wengine wameiomba Jamii kutambua ukatili wa Kijinsia upo hivyo kila mmoja anayonafursa kwa nafasi zao kushiriki kikamilifu katika kupinga na kutokomeza ukatili na ukeketaji mkoani hapa na hatimaye nchi kwa ujumla.
Post A Comment: