Aliyoyasema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
#Rais Dkt. Magufuli ni Baba wa madini kwa sababu kupitia kwake tumefaidika na rasilimali zetu ambazo zamani zilitoroshwa na kuipotezea Serikali mapato na kuiacha nchi kwenye dimbwi kubwa la umasikini.
#Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania unaofanyika leo hii ni wa muhimu kwani unaikutanisha Serikali na wadau wa sekta hiyo pia, ni jukwaa la kuujulisha ulimwengu kuhusu fursa za uwekezaji tulizonazo katika sekta hii.
#Mkutano huu unafanyika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na janga la ugonjwa wa Corona, ni wakati mgumu sana kwa mataifa mbalimbali ila ndani ya nchi yetu tumeendelea kumuomba Mungu huku tukiendelea na jitihada za kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Wizara husika ya Afya.
#Serikali yetu inawakaribisha wadau kuendelea kuwekeza nchini, katika sekta ya madini bado sehemu nyingi za nchi yetu zina hazina kubwa ya madini ambayo hayajaguswa hivyo, kupitia Serikali tunaweza kujenga ubia wa pamoja na wawekezaji katika kufanya biashara hiyo.
#Sekta ya madini inapitia changamoto kutokana na janga la Corona linaloitikisa Dunia lakini Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi tano za wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika.
#Sekta ya madini inaendelea kukua, kufikia mwaka 2025 tunatarajia sekta ya madini itatoa mchango unaofikia asilimia 10 katika Pato la Taifa. Aidha, Mwaka wa Fedha 2020/21, Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 526.7 ambapo katika kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Januari, 2021 Wizara hiyo imeshakusanya shilingi bilioni 360.74
#Mabadiliko ya Sheria ya Madini hayakuwa na lengo la kuwaonea wawekezaji bali kuweka mazingira yenye kutoa taswira yenye uwiano katika mgao wa mapato wa pande zote mbili, tunaahidi kuendelea kushirikiana na wawekezaji wote ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa letu.
#Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo katika sekta ya madini, hivyo inaendelea kubuni na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.
#Natoa rai kwa wachimbaji wadogo na wawekezaji kutekeleza ipasavyo sheria zilizopo, makubaliano mnayoingia na Serikali na kutimiza wajibu wa kurudisha hisani za mashirika yenu kwa wananchi pamoja na kuwapa fursa wananchi waliopo katika maeneo ya migodi.
#Uchimbaji wa madini lazima ushirikiane na wadau wa mazingira, lazima tuangalie tunapochimba madini tuepuke matumizi mabaya ya kemikali kuyeyusha madini na kutiririsha maji yenye kemikali kwenye kingo za maji zinazotumiwa na jamii pia, tuhakikishe hatuachi mahandaki na badala yake tufukie mashimo na kupanda miti.
*Waliyoyasema viongozi wengine*
*Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko*
#Rais Dkt. Magufuli ametoa fursa ya kuchimba madini na kufanya biashara, tuitumie fursa hii kwa uaminifu na kuhakikisha wote tunanufaika na sekta hii, wale ambao ni wachache wanaotaka kuturudisha nyuma tutashughulika nao kwani tunatamani sekta hii iwe rafiki na ifanyike kwa uwazi ili kila aliyewekeza aione faida.
#Yapo matukio ya utoroshaji wa madini yanayoendelea nchini, nalaani matukio haya. Nawaomba wachimbaji wote tuache utoroshaji na badala yake tuangalie mbele kwa sababu hakuna kitu ambacho mchimbaji alikihitaji akakikosa.
#Nawaomba wanaotaka kuleta madini kutoka nchi mbalimbali kuwa tuna masoko yanayofanya biashara hiyo hivyo wafanye biashara kupitia masoko hayo na sio kukutana hotelini.
Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Mark Bristow
#Takriban mwaka mmoja uliopita, Serikali ilitia saini mkataba wa kimataifa wa ushirikiano na kampuni ya Barrick ulioweza kuzaa matunda kwa Serikali ya Tanzania, jamii na wanahisa wa Barrick. Huu ni mfano muhimu wa kuigwa wa pande zote mbili kuweza kunufaika na tumeweza kutoa mfano barani Afrika kwa wawekezaji wote.
#Tanzania ilikuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kuanzisha mkataba wa kisasa wa madini hapo mwaka 1997 kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika tasnia ya madini, Tanzania inaongoza sasa katika kutekeleza uchimbaji na uwekezaji katika madini ambao unaruhusu kuchangia manufaa yatokanayo na madini kwa kupitia ubia na ushirikishwaji wa ukweli.
IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO
Post A Comment: