Na Eleuteri Mangi- WHUSM, Arusha
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameonya watumiaji wa mitandao ya kijamii kinyume na Kanuni ya Maudhui Mtandaoni za 2018 ambazo zinawazuia watumiaji wa mitandao hiyo kutokutumia lugha za kuudhi/matusi na kutokusambaza taarifa za uongo au za upotoshaji.

Waziri Bashungwa amesema hayo jana  jijini Arusha wakati wa kongamano la fursa kwa wanamuziki lililoandaliwa na Taasisi ya kijamii inayoshughulika na wanamuziki (TAMUFO) ambalo jukumu lake ni kuhamasisha maendeleo, kupambana na umaskini, ujinga na maradhi na kuwa na usawa katika mgawanyo wa mapato yanayotokana na muziki kwa wanamuziki.

Ikumbukwe Julai 17, 2020, Serikali ilichapisha mabadiliko ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni kwenye gazeti la Serikali kupitia gazeti Na.29 Toleo la 101 ambayo yalitolewa kupitia notisi Na. 538 yanabadilisha baadhi ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2018 ili kuhakikisha zinalinda maslahi ya watumiaji wa mitandao hiyo bila kuleta taharuki zisizo za lazima katika jamii.

Aidha, Waziri Bashungwa amewataka Watanzania kuendelea kuliombea taifa hatua itakayowasaidia wananchi kuendelea kuwa na afya bora ili kupambana dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Akiongea na wasanii pamoja na wadau waliohudhuria kongamano hilo, Waziri Bashungwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila msanii ananufaika na kazi yake pamoja na kuongeza pato la taifa.

“Nimetoa maelekezo kwa Chama Haki Miliki (COSOTA) wakamilishe mfumo utakaosaidia kutambua kazi za wasanii zinapotumika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wahakikishe kila redio, TV, mabasi, baa ama kumbi za starehe ambao utatambua na kusaidia kukusanya mapato ambayo yatrasaidia wananamuziki kunufaika na kazi zao,” alisema Waziri Bashungwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Kihongosi akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Arusha Iddi Hassan Kimanta amesema mkoa huo upo salama na wasanii kutoka ndani na nje ya mkoa huo wanakaribishwa kufanya kazi zao za Sanaa ili kujiongezea vipato vyao na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Stella Joel na Mwimbaji wa Muziki wa Injili Nchini Tanzania amesema Taasisi hiyo inashirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwapatia wansanii bima ambazo ni mkombozi wa afya zao pindi wanapopata matatizo ya kiafya.

Aidha, taasisi hiyo imewawezesha wanamuziki na wanajamii wapatao 2,014 kupata elimu ya afya na vipimo kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Hospitali za Apollo India na Canada kupitia Excellent International Services Ltd (EIS), Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mt. Meru Arusha, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe na Hospitali ya Wilaya ya Karatu kupitia makongamano yaliyoambatana na uelimishaji na uchangiaji wa damu salama.

Kongamano hili la fursa ni la  nne kufanyika mkoa wa Arusha ambapo hadi sasa jumla ya Kongamano la 27 yamefanyika, kati ya makongamano hayo, yapo yaliyofanya katika mikoa mbalimbali  ikiwemo Dar es salaam, Arusha, Dodoma, Njombe, Mwanza, Morogoro na Iringa.


Share To:

Post A Comment: