Na Ashura Mohamed -Arusha
MWENYEKITI wa wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Arusha ambaye pia ni mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka wametoa pole kwa mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta pamoja na Watanzania wote kwa kuondokewa na mtendaji mkuu wa mkoa huo ambaye ni Katibu Tawala mkoa wa Arusha marehemu Richard Kwitega.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Arusha Taka alisema kuwa taarifa hizo zilipowafikia Jana walipigwa na butwaa kwa kuwa Masaa machache muda wa asubuhi walikuwa katika kikao kazi na Kiongozi huyo kwaajili ya kujadili shughuli mbalimbali za mkoani hapo.
"Ni vile ni kazi ya Mungu haina makosa lakini tumeumia sana juzi Jumapili tulikuwa pamoja hapa ofisini katika Vikao vyetu na wakuu wa wilaya wote na Kiongozi wetu huyu na Jana asubuhi kabla ya kwenda dodoma tumekutana hapa asubuhi ili kuhakikisha tunaweka mambo sawa na yeye anatangulia dodoma kisha sie tutafuata leo maana kikao chetu kilikuwa siku ya Ijumaa ila ndio basi tena tuseme nini sasa, Mungu ameamua kufanya kazi yake."Alisema Taka
Aidha alisema kuwa katibu Tawala alikuwa anatangulia dodoma kwaajili ya kuandaa maandalizi mengine kwaajili ya kikao ambacho kingejumuisha wakurugenzi ,wakuu wa Wilaya na makatibu tawala ambacho kingefanyika siku ya Ijumaa.
Alisema kuwa wapo katika majonzi makubwa na kuwataka Wakazi wa mkoa wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuwa na Moyo mkuu ili kuweza kushirikiana pamoja kuhakikisha kuwa msiba huo na kumaliza salama.
Ametumia fursa hiyo kutoa Pole kwa mkuu wa mkoa wa Arusha bwana Idd Hassan Kimanta kwa kumpoteza mtendaji mkuu wa Ofisi ya mkuu wa mkoa na Kiongozi mahiri ambaye aliweza kuhakikisha kuwa maendeleo ya Mkoa wa Arusha yanakuwa kwa kasi.
Itakumbukwa Marehemu katibu Tawala mkoa wa Arusha Richard Kwitega alifariki dunia Jana majira ya Saa 9:50 Alasiri, katika Ajali ya gari eneo la mizani, Mdori wilayani Babati mkoani Manyara.
Post A Comment: