Tito Mselem na Godwin Msabala Geita,
Imeelezwa kuwa, Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) ina jukumu la kujenga uwezo wa wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni za uziduaji kwa ajili ya kuhoji serikali na kuhamasisha mijadala kuhusu manufaa ya uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia nchini.
Hayo ameyasema, Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Februari 17, 2021, alipokuwa kwenye warsha ya kuelimisha umma na kujadili kuhusu matumizi ya takwimu zilizopo katika ripoti za TEITI mkoa wa Geita ambapo Madiwani, Wachimbaji wadogo wa Madini, na viongozi mbalimbali wa Halmashauri za mkoa wa Geita walihudhulia.
Waziri Biteko amesema kuwa, warsha hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa hususan Madiwani, wachimbaji wadogo, viongozi wa halmashauri na viongozi wa vijiji kwa kuwa mabalozi wazuri kwa kuwajengea uelewa wanachi katika maeneo yao kuhusu kazi na majukumu ya TEITI.
Waziri Biteko amesema, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia, ilijiunga na Asasi ya Kimataifa ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEIT) Februari, 2009 na ilitunukiwa hadhi ya uanachama kamili mnamo Disemba 2012 ili kusimamia utekelezaji wa viwango vya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli zote za uziduaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia.
“Asasi hii inahamasisha wananchi walio katika nchi zenye utajiri wa rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia kuwa na uelewa wa hatua zote zinazohusika katika uziduaji wa rasilimali hizo ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato, na kuwa na ufahamu wa mapato na matumizi ya mapato yanayotokana na rasilimali hizo,” alisema Waziri Biteko.
“Nimeambiwa kuwa hadi sasa tayari TEITI imeshakamilisha na kuweka wazi ripoti kumi (10) zenye takwimu za malipo ya kampuni za madini, Mafuta na gesi asilia kwa kipindi cha Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2018 ambapo ripoti hizo zinaonesha Serikali imekusanya kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.51 sawa na Shillingi Tillioni 8.03 kutoka kampuni za madini, mafuta na gesi asilia,” aliongeza Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amesema, TEITI inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha miundombinu ya utendaji kazi katika sekta hii ya uziduaji ikiwemo uanzishwaji wa masoko ya bidhaa zitokanazo na sekta hii ambapo maboresho hayo yatachangia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya TEITI.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amempongeza Waziri wa Madini kwa usimamizi imara wa shughuli za rasilimali madini katika mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla.
Pia, Mhandisi Gabriel ametoa rai kwa kampuni za uchimbaji wa madini kuendelea kutekeleza Sheria ya uchangiaji huduma kwa jamii na kuhakikisha wananunua vifaa na bidhaa zao ndani ya nchi ili wananchi wanao ishi maeneo ya migodi waweze kunufaika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof Simon Msanjila amesema asasi ya TEITI imeanza kutoa elimu na uhamasishaji kwa wadau wa wa madini ili wajue shughuli za asasi hiyo.
Aidha, Prof. Msanjila amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kutunza takwimu za shughuli zao ili wawe na kumbukumbu ya mwenendo mzima wa shughuli zao kwani itawasaidia kupanga mipango yao ya kimaendeleo na kuisadia Serikali kuwa na taarifa za utendaji kazi wao.
Naye, Mwenyekiti wa TEITI Ludovick Utouh, amesema TEITI inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha miundombinu ya utendaji kazi katika sekta ya uziduaji ikiwemo uanzishwaji wa masoko ya bidhaa zitokanazo kwenye sekta hii.
Utouh amesema, utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya TEITI unasimamiwa na Sheria ya TEITA ya mwaka 2015 ambapo Kifungu Na.10 cha Sheria hiyo kinaainisha majukumu ya TEITI ikiwa ni pamoja na kuboresha uwazi na uwajibikaji hususan katika uvunaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia ili kuongeza manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini.
Aidha, Utouh ameongeza kuwa, TEITI ina jukumu la kuhakikisha kuwa kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia zinaweka wazi taarifa za shughuli zao kulingana na Sheria ya TEITA, 2015.
Pia, TEITI ina jukumu la kujenga uwezo wa wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni za uziduaji kwa ajili ya kuhoji serikali na kuhamasisha mijadala kuhusu manufaa ya uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia nchini.
Utouh aliongeza kuwa, ripoti za TEITI ni nyaraka na nyenzo muhimu sana kwa kuwa zinaweka wazi takwimu mbalibali zinazohusiana na malipo ya kodi na tozo nyingine zinazolipwa serikalini na kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.
Post A Comment: