Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dk Ishmael Kimerei (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya mradi wa FISH4ACP  yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania TAFIRI, Dk Ishmael Kimerei akitoa semina ya mafunzo ya mradi wa kukuza mnyororo wa thamani wa soko la uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa wandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Wandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia semina ya mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu mradi wa FISH4ACP unaotekelezwa kwa ushirikiano wa taasisi hiyo na Shirika la Chakula Duniani FAO.

 KATIKA kuhakikisha wavuvi nchini hasa wale wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wanafanikiwa kufanya biashara zao kwenye mazingira bora, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imekuja na mradi unaoitwa FISH4ACP.


Mradi huo wenye lengo la kuwainua wavuvi hasa wale wadogo wadogo wa Ziwa Tanganyika utatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) ambapo lengo likiwa ni kuongeza mnyororo wa thamani wa samaki wa Ziwa Tanganyika.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam  katika semina ya mafunzo ya siku tatu yanayotolewa na TAFIRI kwa ajili ya kuwajengea uelewa mpana wandishi wa habari juu ya kuripoti mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Ishmael Kimerei amesema kupitia mradi wa FISH 4 ACP wavuvi sasa wa Ziwa Tanganyika wataenda kuboreshewa mazingira yao ya kiutendaji na kibiashara.

Dk Kimerei amesema mpaka sasa wameshapokea kiasi cha fedha Euro Milioni Tatu kutoka kwa wahisani wao ambapo fedha hizo siyo za mkopo kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

 " Tunaamini kupitia mradi huu tutaongeza mnyororo wa thamani wa samaki wa Ziwa Tanganyika kuuzwa kwa uhakika kwenye masoko makubwa nje ya nchi ili serikali iweze kupata kodi yake kikamilifu tofauti na sasa hivi ambapo wafanyabiashara wengi wamekua wakisafirisha samaki hasa wale aina ya Migebuka kwenda nje ya Nchi  kama zawadi lengo likiwa ni kukwepa kodi.

Mradi huu ni wa Serikali na wenzetu wa FAO watakua na kazi ya kutuwezesha na kutusaidia kuukamilish, mpaka sasa kiasi cha euro Milioni 40 kimetolewa kwa Nchi 10 na sisi Tanzania tumepata euro Milioni Tatu na siyo fedha za mkopo hizi, mradi huu utakua ni wa miaka mitano, " Amesema Dk Kimerei.

Kupitia mradi huo wa FISH 4 ACP wavuvi na wafanyabiashara wa samaki kutoka Ziwa Tanganyika watanufaika na kujengewa majiko makubwa ya uchakataji wa samaki na baadae pia kupewa Mafunzo ya jjnsi ya kutengeneza majiko hayo ili waweze pia kujitengenezea wenyewe.

Pia watajenga vichanja bora zaidi vya kuanikia samaki ambazo vitakua na uwezo wa kuzuia samaki kuloa kipindi cha masika ya mvua lakini pia wakijenga miundombinu mizuri ya utengenezaji wa barafu kwa ajili ya kuhifadhia samaki.

Share To:

Post A Comment: