Meneja Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akisoma taarifa wakati wa hafla ya kuzindua rasmi umoja wa wanafunzi wanaochukua fani ya ununuzi na ugavi.
Mgeni rasmi wa hafla ya kuzindua rasmi umoja wa wanafunzi wanaochukua fani ya ununuzi na ugavi mkoani Singida, Kaimu Afisa Vijana wa mkoa huo, Frederick Ndahani (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali. Kulia ni Meneja wa Taasisi hiyo Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Ununuzi na Ugavi wa Taasisi hiyo nchini, Godfred Mbanyi wakifuatilia taarifa ya umoja wa wanafunzi wanaochukua fani ya ununuzi na ugavi. |
Mlezi wa umoja huo, Mhadhiri Msaidizi, Eliaichi Kyara, akifuatilia hafla hiyo. |
Mgeni rasmi akihutubia wanafunzi wanaochukua fani ya ununuzi na ugavi katika Taasisi hiyo ya Uhasibu Tawi la Singida.
Mgeni rasmi Frederick Ndahani (Wa pili kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi na viongozi. Kulia ni Meneja wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema na wa tatu kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Ununuzi na Ugavi wa Taasisi hiyo nchini, Godfred Mbanyi na kushoto ni Mlezi wa umoja huo, Mhadhiri Msaidizi, Eliaichi Kyara na Afisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Samson Julius.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) Tawi la Singida imefungua rasmi umoja wa wanafunzi wanaochukua fani ya ununuzi na ugavi ili kuwaweka pamoja na kutengeneza mahusiano mazuri na bodi ya ununuzi na ugavi (PSPTB)
Akisoma taarifa ya umoja huo wa wanafunzi wanaochukua fani hiyo kabla ya kuzinduliwa Mwenyekiti wa umoja huo Evarist Peter alisema umoja huo uliundwa tangu mwaka 2017 ambapo unajumuisha vyuo 14 hapa nchini vinavyotoa fani hiyo huku wanafunzi wakiwa 590.
"Tunatarajia kupata mafunzo mbalimbali yatakayo tusaidia kukuza ujuzi wetu wa fani ya ununuzi na ugavi ambapo tunatarajia kuleta wataalamu kutoka maeneo na taasisi mbalimbali ikiwemo bodi yetu ya ununuzi na ugavi na wakala wa ununuzi na ugavi (GPSA) na hii ni kwa maslahi yetu na taifa kwa ujumla." alisema Peter.
Mlezi wa umoja huo, Mhadhiri Msaidizi, Eliaichi Kyara alisema lengo la kuanzishwa kwa umoja huo ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi wa fani husika kupata warsha na mafunzo mbalimbali ya ununuzi na ugavi,kuwakutanisha na kuwaweka pamoja wanafunzi wanaochukua fani hiyo hapa nchini,kupata uelewa na kutengeneza mahusiano mazuri na bodi ya ununuzi na ugavi pamoja na kutengeneza fursa ya wanafunzi hao kujiajiri na kuajiriwa.
Kwa upande wake Meneja wa Taasisi hiyo Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema alisema licha ya kuwepo fursa ya chuo hicho mkoani hapo, mwitikio wa wakazi wa mkoa huo ni mdogo kwani wanachuo wengi wanaosoma chuoni hapo wanatoka mikoa mingine.
"Wakazi wa mkoa huu hawachangamkii fursa ya kuwepo taasisi hiyo kwa mamlaka yako tunakuomba uone namna ya kuwahamasisha wazazi ili kuwaleta watoto wao wanaohitimu kidato cha nne na sita nakuomba kwa nafasi yako kuzielekeza halmashauri za mkoa huu kutupatia fursa ya kuendesha mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake ili kuwajengea uwezo kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji wenye tija katika maeneo yao."alisema Mrema.
Akizindua umoja huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Kaimu Afisa Vijana wa Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani aliwaagiza wanafunzi hao kuhamasishana ili wafuate maadili na miiko ya masuala ya ununuzi na ugavi ili wakati wanapopata ajira waweze kuwatumikia watanzania kwa moyo wa kizalendo.
"Bodi ya ununuzi na ugavi endeleeni kuwakumbusha wanafunzi wanaochukua fani hii ili wafuate maadili na miiko mbalimbali ya ununuzi na ugavi awamu hii ya tano kama kuna mtu anafikiri akiajiriwa anaenda kupiga hela hiyo afute nafasi hiyo haipo." alisema na kuongeza.
"Niwaombe wanafunzi kupitia fursa hii mlioipata na mtakapopata ajira serikalini mkasimamie fedha za Serikali,mnao wajibu wa kuisadia jamii kufuata taratibu za manunuzi na ugavi." alisema Ndahani.
Aidha amewaambia kwa kushirikiana na viongozi wa umoja huo atangalia namna na wao kupata nafasi ya kwenda kujifunza masuala ya manunuzi na ugavi katika ofisi ya mkuu wa mkoa ili waendelee kupata uzoefu zaidi wa kivitendo.
Hata hivyo aliwataka wanafunzi hao kubadili fikra kuwa kusoma sio lazima kuajiriwa wanaweza kujiajiri wenyewe kupitia taaluma walioipata,hivyo wafikiri nje ya boksi ili kujikwamua kiuchumi.
"Taaluma ya ununuzi na ugavi ni taaluma muhimu sana kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla hivyo mkaanzishe miradi mbalimbali itakayowasaidia kiuchumi..naamini kwa taaluma yenu mtaisimamia vyema miradi hiyo." alisema Ndahani.
Post A Comment: