Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewataka wapangaji wa nyumba zake wanaodaiwa kodi na kushindwa kulipa kutokana na changamoto mbalimbali kufika ofisi za shirika hilo ili kuangalia namna bora ya kufanikisha kulipa kiasi cha fedha wanazodaiwa kabla ya kuanza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza katika nyumba zake.
Meneja Huduma kwa Jamii wa NHC Bw. Muungano Saguya alisema, baada ya Shirika hilo kuwataka wapangaji wake wanaodaiwa kodi za nyumba zake wawe wamekamilisha kulipa madeni kufikia januari 30 mwaka huu, wapangaji hao wanaodaiwa wameanza kuitikia wito huku wengine wakiwa bado hawajakamilisha kulipa malimbikizo wanayodaiwa.
Akizungumza mbele ya watendaji wa sekta ya ardhi na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma tarehe 24 februari 2021 mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, Bw. Saguya alisema, ni vizuri wale wadaiwa wenye changamoto za malipo wakaenda ofisi za shirika zilizopo kila mkoa na kuonana na watendaji wa Shirika hilo ili kuangalia namna bora ya kulipa madeni yao kwa wakati.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa lina zaidi ya nyumba 17,000 nchi nzima na hadi kufikia Januari 2021 linadai malimbikizo ya zaidi ya bilioni 27 kutoka kwa wapangaji wake ambao wamelimbikiza kodi yao.
“Tulitoa mwezi mmoja hadi tarehe 30 mwezi wa januari ili wadaiwa wote wawe wameshalipa madeni ya kodi ya nyumba na wale watakaoshindwa wataondolewa katika nyumba za shirika na kufikishwa katika vyombo vya sheria” alisema Bw. Saguya.
Alibainisha kuwa baada ya muda waliopewa wadaiwa sugu kuisha shirika limeanza kufanya uchambuzi wa wadaiwa wote ili kubaini mwenendo wa ulipaji wa malimbikizo hayo na zoezi hilo linakamilika mwezi huu wa februari 2021 na mwezi Machi Shirika litaanza kufuatilia wapangaji nyumba hadi nyumba ili kubaini walioshindwa kulipa na wale wenye changamoto ambazo shirika linaweza kukaa pamoja kutafuta ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Bw. Saguya, Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ni za watanzania wote hivyo mpangaji anayeishi katika nyumba za shirika anapaswa kulipa kodi kwa wakati kwa lengo la kuliwezesha shirika kujiendesha lenyewe, kulipa kodi mbalimbali za serikali, kuzifanyia matengenezo nyumba zake na kujenga nyumba mpya kwa ajili ya watanzania wengine wasiopata fursa ya kupanga katika nyumba za Shirika.
Aliwashukuru wapangaji wote waliokuwa wanadaiwa ambao wameweza kulipa kodi kwa wakati baada ya wito wa shirika la nyumba na kusisitiza kuwa nyumba za NHC ni za watanzania wote milioni 50 hivyo uhalali wa waliobahatika kupata upangaji unatokana na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi na kufuata sheria na taratibu za upangaji.
Aidha, Meneja huyo alieleza kuwa mbali na NHC kupangisha nyumba zake imekuwa ikishiriki katika upangaji miji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa hospitali za rufaa za Mwl Nyerere mkoani Mara na ile ya Kanda ya kusini iliyopo Mtwara.
Post A Comment: