Na Tito Mselem, Arusha
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameitaka bodi ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo jijini Arusha kuwa wabunifu ili kukifanya chuo hicho kuwa na tija.
Amesema, Wajumbe wa Bodi hiyo hawajateuliwa kwa bahati mbaya bali waliangaliwa uzoefu wao, taasisi wanazotokea na utendaji wao wa kazi hivyo sifa hizo zikawe chachu katika kuiendeleza TGC.
Ameyasema hayo leo tarehe 13 Februari, 2021 akizindua bodi hiyo ambapo ni bodi ya kwanza kusimamia chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2003.
“Matarajio ya Serikali ni kuona TGC inakua na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa kwa kubuni na kuuza bidhaa za madini nje na ndani ya nchi hivyo kuweni wabunifu ili muisadie TGC kusonga mbele,” amesema Prof. Msanjila.
Pia, Prof. Msanjila amesema kwamba, mwaka 2020 Sekta ya Madini imeongoza kwa kuiingizia Serikali fedha za kigeni na ndiyo sekta iliyoongoza kwa kuuza bidhaa zake nje ya nchi.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa sekta hiyo imekua kwa asilimia 17.7 mwaka 2019 na kuongoza katika ukuaji ukilinganisha na sekta zingine ambapo mchango wake kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.2 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019.
“Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata Sekta ya Madini, bado tuna kazi ya kuhakikisha Kituo hiki kina ongeza udahili wa wanafunzi kwa kupunguza masharti ya sifa za kujiunga na masomo katika Chuo hiki ili tupate wataalamu wengi watakao tusaidia katika shughuli za ukataji, ung'alishani na uongezaji thamani madini,” aliongeza Prof. Msanjila.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TGC, Dkt. George Mofulu ameipongeza Serikali kwa kuwaamini na kuwateua kuwa wajumbe wa Bodi hiyo ya TGC na ameahidi kukisimamia na kukishauri chuo hicho ili kukiletea maendeleo stahiki.
Aidha, Dkt. Mofulu amesema Bodi hiyo itatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Wizara ya Madini ikiwemo suala la sifa ya elimu kwa mwanafunzi ili kujiunga na Kituo hicho, Mchango wa Sekta ya Madini katika Uongezaji thamani Madini pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za watumishi wa kituo hicho.
Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa TGC, Daniel Kidesheni amesema kuwa, Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali za uongezaji thamani madini kwa wadau ikiwa ni pamoja na utambuzi wa madini ya vito, usanifu madini pamoja na uchongaji wa vinyago vya miamba.
Kidesheni, ameongeza kuwa, Serikali imeanza kutumia bidhaa zinazozalishwa katika Kituo cha hicho ikiwa ni kielelezo cha uelewa wa thamani ya bidhaa zitokanazo na madini yanayozalishwa hapa nchini.
Post A Comment: