Na Mwandishi wetu,Mwanza



Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali haitaongeza muda kwa wakandarasi watakaochelewesha au kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji nchini badala yake watanyang'anywa na kutekelezwa na wataalam wa wizara.




 Mhandisi Mahundi amesema juzi  kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela, Mkoani Mwanza.




“Wakandarasi ambao wanachelewesha miradi tutafuatilia ukomo wa mikataba yao na hatutaruhusu muda wa nyongeza labda tu kuwe na sababu za msingi zilizosababisha mradi kuchelewa,” amesema Mhandisi Mahundi.




Aidha amesema kwamba Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote mzembe na kwamba miradi itakayoshindwa kukamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mkataba itakamilishwa kwa utaratibu wa force account.




“Bahati nzuri tunao wataalam wazuri sasa mkandarasi atakayekwenda kinyume na mkataba sambamba na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati, tunamnyang'anya mradi na tutatekeleza wenyewe kupitia wataalam wetu,” alisisitiza Mhandisi Mahundi.




Alisema inasikitisha kuona mkandarasi anashindwa kukamilisha mradi aliyokabidhiwa licha ya  kupewa fedha kama ilivyo kwenye mikataba yake  alisisitiza  Serikali ya awamu ya tano haipo tayari kuendelea kufanya kazi na wakandarasi wa aina hiyo.




“Serikali hii ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya vitendo, suala la mkandarasi kuongezewa muda bila sababu ya msingi hiyo haikubaliki, kwanini mkandarasi awe kikwazo wakati wa kutekeleza miradi licha ya  kunalipwa fedha zake kwa wakati, hii sio sawa,” amesema.




 Mahundi alibainisha  Serikali  imeazimia ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji safi na salama maeneo ya mijini uwe zaidi ya asilimia 95 na maeneo ya vijijini uwe zaidi ya asilimia 85.




Aidha Naibu Waziri amesema   dhamira ya Serikali na Wizara ni kumtua mama ndoo kichwani na hilo litafanyika kwa kuhakikisha huduma ya maji inafikishwa katika kila kaya na siyo kuishia kwenye vituo vya kuchotea maji maarufu kama vioski.




“Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua katika kumkomboa mwanamke na hili litafanyika kwa kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa kumfikishia bomba la maji nyumbani kwake,” alifafanua Naibu Waziri.




Akizungumzia miradi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisuasua na kuiita miradi kichefuchefu hususani kwenye maeneo ya pembezoni ambayo ilikabidhiwa  kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),  Mhandisi Mahundi alithibitisha kuwa utekelezwaji wake unakwenda vizuri na baadhi yake itakazinduliwa mnamo mwezi Machi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji.




Hata hivyo Naibu Waziri wa Maji amepongeza ushirikiano wa viongozi wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela pia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na RUWASA Mkoa wa Mwanza na kuzitaka taasisi zingine kwenye sekta ya Maji kuiga mfano huo.




“Lazima wataalam Sekta ya Maji tuwe na utamaduni wa kujenga mahusiano na Ofisi za Serikali kwenye maeneo ya miradi, ushirikiano nilio uona hapa umenifurahisha na wengine muige kutoka hapa,” alisisitiza Mhandisi Mahundi.




Naibu Waziri Mahundi yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji na alitembelea ujenzi wa mradi wa tanki wa Sahwa, Wilayani Nyamagana pia ujenzi wa tanki  Buswelu Wilayani Ilemela ili kujidhirisha na hatua iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na wasimamizi wake.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: