Tito Mselem na Steven Nyamiti, Dar es salaam
Imeelezwa kuwa, Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa Mwaka 2021 una lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko alipokuwa akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kilichofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar. Es Salaam.
Waziri Biteko amesema kuwa, Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa Mwaka 2021 Madini unaoanza Februari 21, 2021, utahusisha washiriki mbalimbali, Viongozi na Wataalam wa Madini kutoka nchi mbalimbali, Makampuni ya Madini kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia, Waziri Biteko amesema mkutano huo utakwenda sambamba na maonesho ya shughuli za utafutaji, uchimbaji, Uongezaji thamani, biashara ya madini na namna ya uchakataji wa Madini ya Ujenzi na ya Viwandani.
“Pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji tulizonazo kwenye Sekta ya Madini ambao utasaidia kupata wawekezaji katika shughuli za madini, kongamano linaloanza tarehe 21 pia litasaidia kupata maoni kutoka kwa wachimbaji na wadau wengine namna ya kuboresha zaidi usimamizi wa Sekta, Kuwaunganisha kati ya watumiaji wa madini hususan wenye viwanda na wachimbaji wa madini” ameeleza Biteko.
Akiwaeleza Wahariri na Wanahabari kuhusu Mkutano unaoanza tarehe 21, Waziri Biteko amesema kwa Mwaka huu, Wizara ya Madini imeandaa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika kutekeleza Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini kwa kutambua mchango wa mlipa kodi mzuri na wadau walioshiriki vizuri kwa jamii (CSR) hapa nchini.
“Ili kuhamasisha masuala ya uongezaji thamani madini nchini ikiwemo kuwafanya watanzania kutumia bidhaa za mapambo ya madini ya vito yanayopatikana hapa nchini, tumeandaa maonesho maalum ya bidhaa hizo za mapambo ili kueleza kuwa, vitu kama hivi vipo na vinatengenezwa na watanzania hapa hapa nchini,” amesisitiza Biteko.
Pia, Biteko amesema kuwa Mkutano huu utakaoanza tarehe 21 una lengo la kuwaunganisha pamoja Wachimbaji na Watoa huduma katika shughuli mbalimbali zinazofanyika migodini, kuutangazia ulimwengu kuwa Tanzania kuna mazingira mazuri ya uwekezaji sambamba na uwepo wa madini mbalimbali.
Katika kikao cha Wahariri na Waandishi wa habari Waziri Biteko amesema kuwa, Mgeni rasmi siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini huo tarehe 22 Februari, 2021 atakuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku kauli mbiu ya Mkutano kwa Mwaka huu ni “ Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu.
Waziri Biteko ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi kujionea maonesho ya madini yanayoanza tarehe 21 ili watambue madini mbalimbali yanayopatikana hapa nchini, kutambua shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika kwa kampuni kubwa zinazochimba madini, ndogo na za kati ambazo zote zinashiriki maonesho hayo.
Post A Comment: