Na Baltazar Mashaka, Mwanza

WAZIRI wa Madini,Dotto Biteko, amesema ili kujenga uchumi imara,kuchangia pato la taifa na kuleta maendeleo nchini,wachimbaji wadogo wa madini wasikubali kuuza madini ghafi nje bila kusafishwa.

Amesema fursa hiyo inatokana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na mbia wake Lozera kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa kiwango cha kimataifa cha 999.9 chini ya kampuni ya Mwanza Precious Metal Refinery (MPMR) na kuipongeza wizara yake, STAMICO na wabia wake kwa kufanya kazi kubwa ya kuleta teknolojia na uzoefu huo nchini.

Biteko alitoa maagizo hayo jana jijini Mwanza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo eneo la Butuja Katika Manispaa ya Ilemela.

Alisema kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu nchini ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wachimbaji wadogo wa madini na katika kukuza uchumi, kuchangia pato la taifa na kuleta maendeleo,wasikubali kuuza dhahabu ghafi (isiyosafishwa) nje ya nchi, ni lazima iwe imesafishwa.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa kimbilio la wachimbaji wadogo na kitawanufaisha ambapo madini yao ya Silver (Fedha) Zink na Cooper (Shaba) mbali na dhahabu,yatanunuliwa tofauti na zamani ambapo ilinunuliwa dhahabu pekee hivyo soko la madini hayo litakuwepo la uhakika.

“Wizara tunawapongeza sana Bodi na STAMICO kwa kazi kubwa na nzuri pamoja na mbia kukubali kuleta mradi huu nchini na angetamani kuleta mtu wa kusimamia mradi huu maana hatukuwahi kuwa na kiwanda cha kusafisha dhahabu hivyo uwekezaji huu umehamisha uzoefu na teknolojia na kuileta ndani,hivyo tufanye kazi ya kitaalamu  ili mbia naye aonekane,”alisema Biteko.

Aliigiza STAMICO wajiandae kushindana kibiashara na waanze kazi ya kununua na kuzalisha dhahabu wenyewe na wasibwete,wasiponunua dhahabu ndani ya miezi mitatu watafutiwa leseni ili kujenga nidhamu kwa wengine.  

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dr.Venance Mwasse, alisema ujenzi na mtambo huo utakaokuwa na uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa kuanzia,utaweza kupanuliwa hadi kufikia kilo 960 kulingana na upatikanaji wa malighafi, umegharimu sh.bilioni 8.9 ambapo serikali itakuwa na umiliki wa asilimia 25 na mbia asilimia 75.

“Tumekamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa kiwango cha kimataifa cha 999.9 na hadi sasa ufungji wa mtabo umekamilisha bado kufanyiwa majaribio ambapo utaanza uzalishaji Machi 1, mwaka huu,”alisema Dr. Mwasse.

Alisema mtambo huo utaongeza thamani ya madini yanayochimbwa nchini kabla ya kusafirishwa,utaongeza mapato ya nchi kupitia mrabaha (1/3-moja ya tatu),kodi mbalimbali na kutoa ajira 120 kwa Watanzania wakiwemo wageni wachache, wakandarasi,wazalishaji wa dhahabu, wazabuni, wasafirishaji na watoa huduma.

Pia alisema STAMICO imeanza kuainisha maeneo ya upatikanaji wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo kwenye maeneo mbalimbali ya uchimbaji ili kufahamu kiasi cha dhahabu inayozalishwa na kuweza kuwasidia wachimbaji vifaa ili wazalishe zaidi kwa tija na kuuza kwenye refinery.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema uwekezaji huo ni mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kwamba Rais John Magufuli hawezi kufanya kila kitu,hivyo wizara na mwekezaji wamefanya kazi kubwa kutokana na mazingira ya kujikomboa yaliyowekwa na serikali.

Alisema mkoa ulijitahidi kupata eneo la uhakika ili kuwanufaisha wananchi wake na wawekezaji lengo kubwa likiwa ni kuleta thamani ya uchimbaji na kuondokana na kubeba makinikia na kuyapeleka nje ya nchi kama zamani.

Share To:

Post A Comment: