Jeshi la polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata mtandao wa watuhumiwa watatu wa mauaji  ya matukio ya wanawake mkoani Arusha ambayo yamekuwa yakifanyika Mara kwa Mara.


Akizungumza na  waandishi wa habari mkoani Arusha,Kamanda wa polisi mkoani Arusha,Salum Hamduni aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mbise Sanare Lekumo(30) mkazi wa Olasiti ,Lembeka Olomorojo(65)mkazi wa Osunyai na mganga wa kienyeji Bashiri Msuya (64)mkazi wa mtaa wa kirika B kata ya Osunyai jijini Arusha.

Hamduni alisema kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja walihusika katika mauaji ya  mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Anna Edward(44) mkazi wa kata ya Mateves lilitokea januari 25,2021 .

Aidha Kamanda alisema kuwa, watuhumiwa kwa pamoja walimwuua mwanamke mwingine aitwaye Stella Daniel (22) katika tukio lililotokea Mei 21 ,2019 katika eneo la Lolovono,huku tukio lingine likiwa ni mauaji ya mwanamke mwingine aitwaye Bahati Prosper (35),tukio lililotokea januari 16,2020 katika eneo la Ngaramtoni ya chini .

Kamanda alisema kuwa,matukio hayo yote yalisababisha baadhi ya wanawake kuandamana na kufunga barabara januari 30 ,2021 ikiwa ni njia ya kufikisha malalamiko yao kwa serikali ,hali iliyomsababisha kuomba muda na kufanyia kazi malalamiko yao ya tukio hilo la mauaji.

Kamanda alisema kuwa,baada ya kuwahoji watuhumiwa hao walikiri kuhusika na matukio hayo na kuwa sababu zimetajwa kwamba ni imani za kishirikina,na kuwa baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Wakati huohuo jeshi la polisi kwa kushirikiana na kikosi dhidi ya ujangili (KDU) Kanda ya kaskazini kilicho chini ya Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kipindi cha mwaka  2010/2020 kwa pamoja walifanikiwa kukamata silaha 126 Kati ya hizo Magobore ni 125 na Semi _Automatic Rifle Moja zikihusika na makosa dhidi ya wanyamapori.

Kamanda alisema kuwa , watuhumiwa wote  walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa na silaha hizo kutaifishwa.

"baada ya taratibu zote za kisheria  kukamilika silaha zote zinatarajiwa kupelekwa makao makuu ya jeshi la polisi kwa ajili ya taratibu za kuharibiwa ili zisiweze kuingia Tena kwenye shughuli za kihalifu ikiwa ni pamoja na mitandao ya ujangili."alisema Kamanda.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la polisi ,kikosi dhidi ya ujangili na vyombo vingine vya usalama ili kuwafichua wahalifu wanaojihusisha na ujangili na hata wanaoingia katika hifadhi zetu bila utaratibu ili hifadhi hizo ziendelee kuwa salama.

Naye Mkuu wa Kanda ya kaskazini  kikosi dhidi ya ujangili  (KDU) ,Mbanjoko Manyenga alisema kuwa ,kukamatwa kwa silaha hizo ni sehemu ya mkakati ya kupunguza ujangili nchini kwa kushirikiana na jeshi la polisi hasa katika maeneo ya mapori Tengefu ambapo ujangili wa wanyamapori  umekuwa ukifanywa dhidi ya kitoeo.

Manyenga alisema kuwa,kwa Sasa hivi tangu waanze kukamata silaha hizo ujangili umepungua Sana ,hivyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo hivyo huku wakiacha kujihusisha na matukio hayo.


Share To:

Post A Comment: