Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekerwa na halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuandaa Hati za Ardhi nne katika kipindi cha miezi nane tangu kuanzishwa kwa ofisi ya Ardhi mkoa wa Ruvuma.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utoaji hati katika halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma ambapo katika kipindi cha miezi nane halmashauri za mkoa huo zimeandaa jumla ya hati 623.
Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma tarehe 24 Februari 2021 katika kikao kazi cha kuzungumzia masuala ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alisema haiingii akilini halmashauri kuandaa hati nne kwa miezi nane huku halmashauri hiyo ikiwa na watendaji wanaolipwa mishahara.
Alisema, katika kuhakikisha halmashauri za mkoa wa Ruvuma zinaongeza kasi ya utoaji hati ni lazima wakurugenzi wa halmashauri hizo kuwawekea malengo watendaji wa sekta ya ardhi ya kuandaa hati zisizopingua tatu kwa wiki kwa kila mtumishi.
‘’Uandaaji hati ufanywe na watendaji wote wa sekta ya ardhi kwa kupeana malengo ya kila mtumishi aandae hati ngapi, kwenye halmashauri mtumishi anaweza kuanza na kuandaa hati 5 au 3 kwa wiki na mkifanya hivyo mnaweza kuandaa hati nyingi’’ alisema Dkt Mabula.
Taarifa ya Sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma iliyowasilishwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa Ildefonce Ndemela ilieleza kuwa, jumla ya hati 623 ziliandaliwa na halmashauri za mkoa wa Ruvuma tangu kuanzishwa ofisi ya ardhi mkoa Machi 2020. Alitaja idadi ya hati zilizoandaliwa kwa kila halmashauri kuwa, ni halmashauri ya wilaya ya Mbinga hati 52, Mbinga Mji 153, Manispaa ya Songea 249, halmashauri ya wilaya ya Namtumbo hati 4, Madaba 16, Songea 34, Nyasa 82 na Tunduru 33.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, baadhi ya halmashauri katika mikoa mingine zimekuwa zikifanya vizuri katika kuandaa hati ambapo halmashauri mmoja huandaa hati 300 kwa mwezi na kutolea mfano wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika mkoa wa Mwanza kuwa imekuwa ikiandaa hati 300 hadi 350 kwa mwezi.
Dkt Mabula aliziagiza idara za ardhi katika halmashauri za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha zinampatia taarifa ya utekelezaji maagizo aliyoyatoa yakiwemo makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, ufuatiliaji wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi pamoja na utoaji wa hati za ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameonesha pia kutoridhishwa na hali ya makusanyao ya kodi ya pango la ardhi kwa mkoa wa Ruvuma ambapo hadi sasa mkoa huo umeweza kukusanya shilingi 740,775,023.00 sawa na asilimia 16 kati ya malengo ya kukusanya bilioni 4.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa huo tarehe 24 Februari 2021. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Ruvuma Ildephonce Ndemela
Sehemu ya wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa huo tarehe 24 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Songea aliowakabidhi hati za ardhi wakati wa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Ruvuma tarehe 24 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa Ramani ya Mpango wa eneo la Lilambo katika Manispaa ya Songea na Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa hiyo Saidy Msananga wakati wa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Ruvuma tarehe 24 Februari 2021. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)
Post A Comment: