Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (katikati) akitoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa akipatiwa matibabu ambapo aliwataka Watanzania kuendelea kuziamini hospitali za Serikali nchini kwa kuwa zimesheheni wataalam wabobezi, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Alphonce Chandika.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (kulia) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma ambapo aliahidi kuelekeza nguvu zake kumshauri Mheshimiwa Rais kuwekeza katika huduma za Afya, kushoto ni Kiongozi wa Jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia katika hospitali hiyo, Dkt. Anthony Yunda.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma, Dkt. Alphonce Chandika (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) muda mchache baada ya kuruhusiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango akiushukuru uongozi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma kwa huduma nzuri waliyompatia na Watanzania wote kwa ujumla kwa kumuombea wakati wote alipokuwa akiugua, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Alphonce Chandika.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa karibu mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango muda mfupi baada kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma.
(Picha na Wizara ya Fedha na Mipango, Dodoma)
…………………………………………………………………………………….
Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango amewataka Watanzania kuendelea kuziamini hospitali za Serikali nchini kwa kuwa zina wataalam waliobobea katika kutibu magonjwa mbalimbali.
Alitoa wito huo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari akiwashukuru watanzania kwa kumwombea na kumtakia heri ya afya njema muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa alipokuwa akipatiwa matibabu.
Ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa pamoja na watumishi wake kwa huduma nzuri walizompatia na kufafanua kuwa uzalendo wao wa kuhudumia wananchi kwa moyo wa dhati unastahili kuigwa.
“Nataka niwaambie watanzania kuwa afya yangu imeimarika kabisa na hatimaye jopo la madaktari wameona nina afya njema na nina uwezo wa kutoka kurudi kuendelea kulitumikia taifa letu, nawashukuru sana madaktari, wauguzi, na wahudumu kwa kunihudumia kwa upendo na moyo wa dhati. Mungu awabariki.”alisema Dkt. Mpango
Alisema hakuna sababu ya watu kukimbilia Ulaya kwenda kupata matibabu kwa kuwa hospitali zilizopo nchini ikiwemo ya Benjamin Mkapa zina vifaa vya kisasa na wataalamu wa kutosha jambo la msingi ni kuziimarisha ili wananchi wengi wanyonge wapatiwe huduma stahiki.
Dkt. Mpango alielezea furaha yake kuwa katika kipindi chake cha uongozi katika Wizara ya Fedha na Mipango huduma za afya zimepewa kipaumbele na kuongezewa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, vifaa na kusomesha wataalamu na kubainisha kuwa ataendelea kumshauri Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aendelee kuboresha sekta hiyo.
Alitoa salamu za shukrani kwa Mheshimwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, viongozi mbalimbali pamoja na watanzania kwa ujumla kwa salamu na maombi yao, amethibitisha kuwa afya yake imeimarika na ameshaanza kufanya kazi hata akiwa bado hospitali kabla ya kuruhusiwa baada ya kupona.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na familia yake kwa kunijali na kufuatilia afya yang una kuniombea kila siku, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kasim Majaliwa, Spika Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma, viongozi wa dini, wananchi na watu wengine wote. Wamefanyakazi usiku na mchana. Asanteni sana”aliongeza Dkt. Mpango.
“Kwa wale wanaotembelea Benki watakuwa mashahidi kwa kuwa wameona kitu (mshahara) leo”akiwa na maana kuwa likuwa ameidhinisha kutoka kwa mshahara akiwa hospitalini
Aidha, Dkt. Mpango ameungana na Watanzania kuomboleza vifo vya watu mbalimbali waliopoteza Maisha wakiwemo Viongozi, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi Dkt. John Kijazi, Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servicius Likwelile na Aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambaye pia alikuwa mwalimu wake, Prof. Beno Ndulu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika alisisitiza Watanzania kuwa wazalendo na kuachana na tabia ya kueneza vitu wasivyokuwa na uhakika navyo mitandaoni kwa kuwa mitandao imeandika mambo mengi lakini leo Mhe. Dkt. Mpango ameruhusiwa akiwa na afya njema tayari kwa kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Alitoa shukrani kwa Serikali chini ya Uongozi mahili wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuboresha miundombinu ikiwemo vifaa tiba vya kisasa pamoja dawa katika hospitali hiyo na kwamba wao kama wataalam kazi yao kubwa ni kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Post A Comment: