Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Advocacy for Health and Development (AHEAD) Tanzania limegawa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule tatu za msingi katika kata ya Shambarai iliyopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5
Vifaa hivyo ni taulo za kike ambazo wanafunzi hao wanaweza kuzifua baada ya kuzitumia, nguo za ndani kwa wanafunzi wa kike, madaftari, kalamu, penseli na vifutio kwa wanafunzi wa darasa la nne.
Shule zilizopata msaada huo ni pamoja na shule ya Msingi Shambarai, Kandaskrai na Nakwani.
Akizungumza mara baada ya kukamibidhi misaada hiyo mkurugenzi mkuu wa AHEAD Leila Mushtaq alisema shirika hilo lina mpango wa kuwafikia wanafunzi wa kike zaidi ya 5000 ili kukabiliana na changamoto ya utoro unatokana na kukosa taulo za kike wakati wa kupata hedhi.
"Zoezi hili ni endelevu.Tunajua changamoto wanayopata wanafunzi wa kike ya kukosa taulo za kike za kutumia wakati wa hedhi haswa kwa wale wanotoka maeneo ya vijijini na ndiyo sababu tumejikita kugawa taulo hizi zinazaweza kutumika kwa miaka mitatu bila kuleta mashara yeyote kwa watumiaji".
Naye Vicky Ulomi kutoka AHEAD Tanzania ametumia fursa hiyo kuwaomba watu wenye mapenzi mema pamoja na mashirika mbalimbali kutoa msaada wa vifaa vya mbalimbali kwa wanafunzi wa jami hiyo ili waweze kupata elimu.
Wakizungumza kwa furaha mara baada ya kukabidhiwa taulo hizo Gift John, Agape Mollel na Neema Immanuel walisema wanaushukuru uongozi wa AHEAD kwa msaada huo wa tulo za kike na nguo za ndani kwani awali walikuwa wankabiliwa na adha kubwa ya kukosa taulo hizo.
Tunashukuru kwa msaada huu.Ni zawadi nzuri kwetu kwa sababu hatukuwa na uwezo wa kupata taulo za kike kwa sababu huku ni kijijini na wazazi pia hawana uwezo wa kutununulia".
Amesema mara nyingi wakiwa kwenye hedhi walikuwa wanakatisha masomo kutokana na hofu ya kuhofia kuchafuka darasani lakini sasa taulo hizo zitawasaidia na kuwafanya wawe jasiri na wenye furaha wakati wa hedhi kwa kwenda bila kihofia kuchafuka.
Amesema walikuwa wanatumia vitabaa vya kanga ambavyo siyo salama na kwamba baadhi ya wanafunzi hawakiwa na uwezo hata wa kupata vipande hivyo kwa ajili ya kujistiri.
Mwalimu Ester Elisafi anayeshughulika na masuala ya wanafunzi wa kike katika shule ya msingi Nakwani alisema hedhi ilikuwa inasababisha utoro kwa wanafunzi wa kike kwa sababu ya kukosa taulo za kike.
"Wanafunzi wengi wakati wa hedhi huwa hawaji shuleni na hata ukiwauliza ni vigumu kuniambia ukweli kuwa alibaki nyumbani kutokana na hedhi".
Amesema jamii ya kifugaji mila na desturi zao zonawaathiri wanafunzi wa kike haswa wakiwa kwenye hedhi kwa sababu huwa wanakatazwa na wazazi kuwaambia waalimu hivyo wakati mwingine wanapata wakati mgumu kuwasaidia.
Amesema mahitaji ya taulo za kike kwa wanafunzi wa kike haswa wanaotoka jamii ya kitugaji ni makubwa na kuomba uongozi wa AHEAD kuzifikia shule nyingi zaidi zilizopo katika jamii hiyo.
Ester aliushukuru uongozi wa AHEAD Tanzania kwa elimu waliyoitoa kwa wanafunzi hao wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao tofauti na awali ambapo walikuwa hawajapata elimu jinsi ya kutumia taulo za kike na athari za ndoa za utotoni.
Post A Comment: