Najua wengi mmeumia sana. Mmestaajabishwa mno na maamuzi ya Chama changu cha ACT wazalendo kukubali kuungana na Serikali ya Magufuli na Mwinyi tuliyoitangazia dunia imeunajisi Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.
Kitendo cha Chama kukubali kupeleka jina la Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, na kuridhia kuapishwa wabunge wake; naelewa na naona wengi wananchi wenzangu si tu kimewakasirisha kupitiliza ila bali pia kimewatolea imani katika kuwaamini wanasiasa na vyama vya upinzani nchini.
Wengi tangu Jana Desemba 06, 2020 Chama kilipotangaza uamuzi wake huo kupitia Katibu Mkuu, rafiki yangu Ado Shaibu mmeendelea kuniuliza msimamo wangu mtandaoni, kwa simu hadi ana kwa ana kwa kuzingatia mimi kama mwanachama na Mtanzania ninayependa na kuheshimu Haki za Binadamu na Demokrasia, hivyo hakika nasema hampo peke yenu, Masikitiko yenu Watanzania wenzangu ni masikitiko yangu pia.
Uchaguzi ulikuwa batili, uongozi uliopatikana na unaoendelea kupatikana na uchaguzi huu ni batili pia. Haramu haijawahi kuwa halali. SIMPLE MATHEMATICS.
Kwangu mimi Suphian, ndoto yangu kuu ya kuona Taifa langu huru na lenye kufuata misingi ya Haki ni Lulu zaidi ya maslahi ya Chama cha siasa nilipo au yeyote ninayemwamini katika Siasa au nje ya siasa.
Kama nilivyoahidi wakati wa Sakata la Wabunge 19 wa CHADEMA, kwamba siwezi kumumunya maneno pale haki ikipindishwa hata kama na Chama changu, hivyo NATANGAZA: SIUNGI MKONO MAAMUZI YA CHAMA CHANGU.
Hivyo naomba dunia ijue kuanzia Leo Desemba 07, 2020 mimi Suphian Juma Nkuwi rasmi NANG'ATUKA UANACHAMA wa ACT wazalendo ili kusimama na HAKI, kusimama na familia za ndugu waliouawa, kutekwa, kufungwa na kuumizwa wakipigania Uchaguzi Huru, Haki na unaoaminika.
Asante Kiongozi wa ACT wazalendo na Kaka yangu, Zitto Kabwe na Chama kwa ujumla kwa malezi yenu ya KUSIMAMA NA HAKI mliyonipatia tangu mwaka 2015 nilipojiunga nanyi, nawatakia kila kheri.
Suphian Juma,
Aliyekuwa Mgombea Ubunge, ACT wazalendo 2020-2025 Singida Magharibi.
Desemba 07, 2020.
Post A Comment: