Rais Magufuli amesema atafanya uteuzi mpya wa Naibu Waziri wa Madini baada ya aliyemteua, Francis Ndulane kushindwa kuapa.
Amesema hayo leo Jumatano tarehe 9 Desemba 2020, muda mfupi baada ya kumaliza kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, wakati akichambua wizara moja baada ya nyingine pamoja na mawaziri na naibu wao.
“Tumeangalia nafasi ya mikoa, ndiyo maana tumekuja na ninyi na tuna akiba nyingi sana kwa hiyo tukibandua tu, tunabandika kingine. Ninawaomba mkajitume sana na kuwatumikia wananchi. Tume-balance wazee na vijana. Kuna mzee George Mkuchika ambaye amekuwamo wakati wa Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Hata mimi kwenye baraza nataka wazee na hata ushauri wao na lazima tuzitunze hazina zetu.
“Ninawafahamu wote niliowateua, mpaka wewe uliyeshindwa kuapa. Nafikiri nitamtafuta mwingine anayejua kuapa vizuri. Waziri Mkuu ananiangalia kwa sababu Lindi wametoka yeye na huyu aliyeshindwa kuapa, sasa tutamteua mwingine na wewe tutacheki digrii yako vizuri. Tunakupongeza utaendelea kuwa mbunge,” amesema Rais Magufuli.
“Kuna Mbunge tulimfukuza kwenye vyeti feki leo ameenda ametamba na kawa Mbunge, ila kwa kuwa ‘qualification’ ya Ubunge ni kusoma na kuandika, na wewe uliyeshindwa kuapa tutachunguza vyeti vyako na tutamteua mwingine” alisema Magufuli.
Rais Magufuli amesema, lazima kuwe na naibu waziri anayeweza kusoma vizuri nyaraka mbalimbali ili asije kusaini nyaraka za muhimu bila kusoma kwa umakini.
Wakati wa kiapo, Kumba alikuwa akikosea kusoma kiapo kwa kurudia rudia hali iliyomfanya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kumpa maelekezo.
Hata hivyo, Ndulane ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM) hakumaliza kiapo chake kwa Balozi Kijazi kumwomba aende akampumzike kwanza ili kupisha wengine kuendelea kuapishwa.
Kwa mujibu wa wasifu wa Ndulane uliowekwa katika tovuti ya Bunge la Tanzania, inamwonyesha ana shahada ya uzamili ya uhasibu na fedha aliyoipata Chuo Kikuu cha Mzumbe kati ya mwaka 2013 hadi 2015.
Post A Comment: