Na Angela Msimbira SUMBAWANGA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe David Silinde amewaagiza Viongozi wa Mikoa yote nchini kuhakikisha zoezi la ujenzi wa madarasa linakuwa endelevu na kuwekewa mikakati maalum ili kupunguza uhaba wa madarasa nchini.
Ametoa agizo hilo leo wakati akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa ambapo Mhe. Silinde amesema zoezi la ujenzi wa madarasa si la kushitukiza, hivyo ni vyema viongozi wote ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka mikakati madhibuti ya kuhakikisha madarasa yanajengwa kwa wakati.
“Haiwezekani kila mwaka tunajua idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi lakini bado tunakuwa na uhaba wa madarasa nchini, hali hii inapoteza haki ya watoto waliofaulu vizuri mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza” amesisitiza Mhe. Silinde
Mhe. Silinde anafafanua kuwa Serikali itahakikisha inakagua na kujiridhisha utoshelevu wa madarasa kwa watoto wote waliofaulu Mitihani ya kumaliza shule ya msingi na kuwa watahakikisha kuwa wanapangiwa shule.
Amesema Serikali hahitaji maneno mengi kinachohitajika ni kuwa madarasa yamekamilika, kwa kuwa, watoto kujiunga na Kidato cha kwanza si jambo la dharura, hili ni jambo linalofahamika katika kipindi chote, hivyo udharura huihitajiki katika miaka mingine inayokuja “amesisitiza Mhe. Silinde
Mhe Silinde amesema kuwa zoezi la ujenzi wa madarasa linatakiwa kuwa endelevu na kuhakikisha kuwa hakuna uhaba wa madarasa kulingana na wanafunzi wote wanaoongezeka kila mwaka.
“Inafahamika kuwa kunaongezeko kubwa na wanafunzi kila mwaka, wanafunzi wanaofuatia kwa mwaka mwingine, pia ongezeko la idadi ya watu kila mwaka katika taifa letu, hivyo kila Mkoa uhakikishe unajipanga na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua tatizo la madarasa” amesema mhe. Silinde
Mhe. Silinde ametoa Rai maeneo yatakayoonekana na upungufu mkubwa wa madarasa, vifaa ikiwemo madawati Serikali haitasita kuwachukulia hatua viongozi wa eneo hilo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inafuatilia na kuhakikisha hakuna muda wa kupumzika katika kipindi chote mpaka watoto wote waliofaulu na kuchagulliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanasoma madarasani
Wakati huohuo Mkuu wa Wilaya ya Sumabawanga Mhe. Halfani Haule amesema mpaka sasa Halmashauri hiyo imejipanga kukamilisha maboma ya madarasa yaliyopo lengo likiwa kuhakikisha watoto waliofaulu elimu ya msingi wote wanachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na wanakaa darasani
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mwl. Nyangi Msema kweli amesema kuwa Halmashauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 57 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya shule ili kuhakikisha wanafunzi zaidi ya 4400 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaingia darasani ifikapo januari, 2021.
Post A Comment: