Mkuu wa wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala (kushoto) akikabidhiwa mifuko ya saruji 100 na Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza Road kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kanyonza
Moja ya madarasa ya shule za sekondari jimboni humo.
MBUNGE wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kamamba, amekabidhi mabati 300 yenye thamani ya sh.milioni 9 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mabati hayo, Kamamba alisema ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kutatua changamoto mbalimbali.
"Niliahidi kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika jimbo letu na nimeanza na changamoto za miundombinu kwa kununua mabati 300 kwa ajili ya ujenzi wa shule zetu" alisema Kamamba.
Alisema mabati hayo yatapelekwa kujenga miundombinu katika shule tatu za sekondari katika jimbo hilo.
Alizitaja shule hizo kuwa ni Sekondari ya Kanyonza iliyopo Kata ya Kanyonza ambayo itaipata mabati 100, Shule ya Sekondari Kakonko ambayo nayo itaipata mabati 100 na Shule ya Sekondari ya Ushindi iliyopo Kata ya Kasuga.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala akikabidhiwa mifuko ya saruji 100 na Kampuni ya Ujenzi ya Nyanza Road kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kanyonza ikiwa ni maandarizi ya kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza Januari 2021 aliushukuru uongozi wa kampuni hiyo na kumpongeza mbunge huyo kwa kuanza kwa kasi kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chamsingi hicho ya 2020/ 2025.
"Nikupongeze mheshimiwa mbunge kwa kuanza kutekeleza ilani ya chama chetu na sisi kama Serikali tutakupa ushirikiano wa kutosha" alisema.
Mwananchi wa Kata ya Kasanda, Alexander Madebwa amemshukuru mbunge huyo kwa juhudi za maendeleo alizoanza kuzifanya hasa katika kuboresha miundombinu upande wa elimu.
Mkazi wa Kata ya Kanyoza Shetiel Juma amempongeza mbunge wao kwa hatua hiyo aliyoianza ambayo inaleta natumaini mapya kwa wananchi wa jimbo hilo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kakonko, Abdul Kambuga Amempongeza mbunge huyo kwa kuanza kwa kasi utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na kuwa kasi hiyo inawafanya wananchi kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na chama hicho chini ya Rais Dkt.John Magufuli.
Post A Comment: