MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameendelea na ziara yake jimboni humo ambapo ametembelea miradi minne ya ujenzi wa miundombinu ya elimu yenye thamani ya Sh Milioni 196 inayotekelezwa na serikali katika shule ya sekondari ya Unyahati.
Miradi hiyo ni ujenzi wa bweni moja,madarasa matatu,maabara tatu na matundu sita ya vyoo.
Pamoja na kutembelea miradi hiyo,Mtaturu ametimiza ahadi yake aliyowahi kuitoa kwa shule hiyo ya kupeleka mashine ya kuchapa (Printer) moja yenye thamani ya zaidi ya Sh laki tano inayofanya kazi ya kuchapa,kunakili na kuskani.
Akizungumza Disemba mosi 2020, akiwa katika ziara hiyo Mtaturu amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kuwapelekea fedha zilizofanikisha ujenzi huo.
“Katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM iliyopita na hii ya sasa imeeleza dhamira ya kuboresha miundombinu ili kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishia,kwa niaba ya wana Singida Mashariki nimshukuru Rais Dkt Magufuli kwa kuleta fedha maana kuahidi ni jambo moja lakini kutekeleza ni jambo la pili,Rais wetu ametekeleza,”alisema.
Amesema mbali na kutoa fedha hizo amewezesha upatikanaji wa elimu bila ya malipo na hivyo kupelekea uwepo wa mafanikio mbalimbali ikiwemo ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa na ongezeko la ufaulu.
Ili kuunga mkono juhudi hizo za serikali Mtaturu ametimiza ahadi yake aliyowahi kuitoa ya kuwapa motisha wanafunzi watano waliofaulu kwa daraja la kwanza kwa kuwapa Sh laki moja kila mwanafunzi na walimu waliopelekea uwepo wa ufaulu huo.
“Niliahidi kuunga mkono juhudi za serikali,na katika vipaumbele vyangu saba nilivyoahidi kuvisimamia kipaumbele cha kwanza ni katika sekta ya elimu,na hapa nimesema nitakuwa kinara katika kusimamia sekta hii kwa kushirikiana na serikali,na sasa natimiza ahadi yangu ya kutoa Sh laki moja kwa kila mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ambao sasa hivi wapo kidato cha tano,hivyo nakabidhi Sh laki tano,
“Najua mafanikio haya ya wanafunzi hayajaja yenyewe,bali yametokana na juhudi za walimu wetu,niliahidi na natimiza ahadi yangu ya kuwapa Sh laki moja kwa walimu wote kama njia ya kuwapongeza kwa kuwawezesha vijana wetu kufanya vizuri,na hii ni motisha ili mfanye vizuri zaidi ya mlivyofanya sasa,”alisema Mtaturu.
Amehimiza mshikamano katika suala zima la ufundishaji ili kuendelea kuboresha taaluma.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa shule hiyo mwalimu mkuu Method Njiku amemshukuru Rais Magufuli kwa fedha alizopeleka na kumshukuru pia Mbunge Mtaturu kwa uthubutu wake wa kuwashika mkono kwa kile walichoonyesha.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Unyahati Abeli Surri amemshukuru mbunge huyo kwa kuwatembelea na kusema miaka yote kumi ya udiwani wake hajawahi kutembelewa na mbunge.
"Mbunge wetu tangu umeingia bungeni umekuwa ukitusemea kero zetu na matunda yake tunayaona miradi mingi tunaipata,ahsante sana,"alishukuru diwani huyo.
Post A Comment: