Mratibu wa dhana ya Afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu  Harrison Chinyuka  akifungua mkutano mkuu wa 37 na Kongamano la Kisayansi la Chama cha Wataaamu wa Afya ya Jamii Tanzania (TPHA)  jijini Arusha jana,
Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Philbert Nyinondi akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.
Mwenyekiti Mteule wa TPHA Dkt. Mariam Ongara akitoa shukrani kwa mgeni rasmi mara baada ya kufungua mkutano huo.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa  wa Arusha, Hergeberg Chitukuro akitoa salamu za mkoa huo kwa wajumbe wa mkutano huo.
Magreth Orumbe akiimba wimbo wa kumsifu Mungu mbele ya wajumbe kabla ya kutoa sala ya kuukabidhi mkutano na majadiliano hayo kwa Mungu kwa ajili ya siku zote nne watakazokuwa mkoani Arusha.
Prof.Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akichokoza mada kwenye kongamoano hilo kuhusu Hatari,Athari,Utayari na Jinsi ya kujilinda na Magonjwa ambukizi.
   Muwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Ritha Njau akiwasilisha mada ya pili kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 na changamoto zake.
Mwenyekiti wa chama TPHA  Dkt. Philbert Nyinondi akimtambulisha mwenyekiti Mteule Dkt.Dkt. Mariam Ongara (anayepungia mkono)

Wanachama na wajumbe wa mkutano na kongamano hilo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa. 


Na. Calvin Gwabara, Arusha.

PAMOJA na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, watafiti na wadau wengine wa maendeleo katika kuyakabili magonjwa ambukizi na yasiyoambukizi na usugu wa vimelea vya magonjwa lakini bado bado yameendelea kuwa  changamoto kubwa nchini.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa dhana ya afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu  Harrison Chinyuka wakati akifungua mkutano mkuu wa 37 na Kongamano la Kisayansi la Chama cha wataaamu wa afya ya jamii Tanzania (TPHA) jijini Arusha.

Alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za uchumi wa kati lakini nayo ipo katika hatari ya kupatwa na magonjwa hayo na kuathiri jamii hivyo mkutano huo ni muhimu sana kujadili vichocheo vya magonjwa hayo na jinsi ya kuyakabili .

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ambukiza katika jamii yetu kama vile magonjwa ya moyo,kisukari,kansana mengineyo hivyo nina imani kuwa wataalamu mlio hapa mnafahamu kuwa magonjwa haya yamekuwa tishio kubwa pia kwa jamii na kuhatarisha uchumi wa nchi kwa ujumla tumieni nafasi hii kujadili kwa pamojajinsi ya kuyakabili na athari zinazotokana na magonjwa haya” Alisisitiza Chinyuka.

Mratibu huyo wa dhana ya afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi ya afya za Binadamu,Wanyama na usugu wa vimelea vya magonjwa lakini Wizara,Idara na wakala mbalimbali wa Serikali na za binafsi kila mmoja imekuwa ikipambana na namna yake mmojammoja lakini ili kupata ufanisi mkubwa wa kuzuia,kujiandaa na kuakabili lazima dhana ya afya moja itumike ili kuwa na nguvu ya pamoja.

“Dhana ya afya moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea vingi vinavyosababisha magonjwa kwa binadamu vinatokana na wanyama na kasi ya maambukizi inaongezeka pale binadamu anapoingilia makazi ya wanyama hao katika mazingira yao bila tahadhari” Aliongeza Chinyuka.

Alibainisha kuwa hali ni hatarishi zaidi kwa bara la Afrika kwa kuzingatia kuwa bara hili hususani sehemu zinazokaribia misitu mikubwa ya Kongo yenye wanyama wengi wa aina mbalimbali na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko kama vile Ebola,Homa ya bonde la Ufa,Marburg na mengineyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo wa kisayansi, Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Philbert Nyinondi alisema kuwa chama hicho kiliundwa mwaka 1980 kwa lengo la kufanikisha vita dhidi ya  adui maradhi dira ambayo bado wanaendelea kuiishi.

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha wanajenga taifa na dunia iliyo salama chama hicho kimeshiriki kikamilifu kutoa elimu kwa Umma,kushauri sera,sheria na kanuni bora katika kuimarisha afya ya jamii,kushirikiana na Serikali na washirika wa maendeleo katika utekelezaji wa mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha afya ya jamii pamoja na kuandaa majukwaa ya wadau na kutoa fursa kwao kutoa mchango wa kimawazo na kimkakati kuimarisha afya.

“Tunajivunia miaka 40 ya utendaji kazi wa chama chetu bila kuwa na migongano na serikali za awamu zote tano  na sisi wana TPHA tunaungana na Rais wetu Dkt. John  Magufuli katika nia yake ya kuimarisha na kujenga miundombinu mipya ya afya kwani imeimarisha huduma za afya nchini” alibainisha Dkt. Nyinondi.

Alisema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau kushiriki kikamilifu kutathimini mafanikio makubwa waliyoyapata,kujipanga na kuiandaa jamii kwa magonjwa ya mlipuko na yanayoibuka na kuishauri Serikali na ulimwengu namna bora ya kukabiliana na  milipuko taraji na siayotarajiwa bila kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya watu.

Akitoa shukrani kwa mgeni rasmi Katibu wa TPHA Dkt. Mariam Ongara alisema wao kama chama watayafanyia kazi yale yote yaliyoshauriwa na mgeni rasmi hususani dhana ya afya moja  ili kuweza kuingeza tija katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukizakwa maslahi mapana ya jamii na Taifa.

Alibainisha kuwa wao kama chama wanafanya kazi kwa kufuata miongozo na taratibu zote za serikali na zinazosimamia masuala ya afya na kuisaidia serikali kufikia malengo yake kwa kufanya tafiti na kushauri njia bora ambazo zinafaa kutumika katika kuimarisha afya za watu.

Akiwasilisha mada ya kwanza iliyobeba mkutano huo Profesa. Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  alisema kuwa awali ilionekana tatizo la magonjwa ya kuambukizwa na mlipuko ni ya Afrika,China na kwenye maeneo ya misitu ya Amazon  pekee lakini sasa ni dunia nzima na hii ni kutokana na kurahisishwa sana kwa njia za usafiri na hivyo kusamnbaza magonjwa hayo kirahisi.

Prof.Mdegela alisema tafiti zinaonyesha magonjwa hayo mengi ya milipuko na kuambukizwa yanatokana na Wanyama ambao sio binadamu kama vile nyani,Sokwe na Ngedere, Popo na Panya wanyama ambao wapo kila kona ya Tanzania na jamii inaishi nao wengine bila hata kuchukua tahadhari.

Alisema kuna mambo kadhaa ya kufanya ikiwemo kuangalia kama utaalamu na taaluma hiyo ipo nchini ya kutambua magonjwa hayo na kisha kujulisha umma uwepo wa magonjwa hayo kwani kuna maeneo ambayo wasambazaji wa magonjwa hayo ni kitoweo kwao kama vile panya. 

Mkutano na Kongamano hilo la kisayansi la chama Cha Wataalamu wa Afya ya Jamii Tanzania (TPHA), umebeba Mada isemayo “Magonjwa ambukizi yanayojitokeza na yale yanayojirudia: Hatari,Athari,Utayari na Jinsi ya Kuyakabili” 

Share To:

Post A Comment: