Na. Majid Abdulkarim, Dodoma


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameelekeza ifikapo Desemba 20 mwaka huu Hospitali ya Uhuru iwe imeshaanza kutoa huduma ili kutekeleza adhima ya serikali ya kusogeza huduma za afya kwa wananchi.


Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo wakati akikagua umaliziaji wa ujenzi wa Hospitali hiyo unaoendelea katika wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma.


Akizungumza Mhe. Majaliwa amesema kuwa vifaa vyote vinavyotakiwa pamoja na samani, vifaa tiba vinavyotakiwa kuwepo kwenye hospitali hiyo vipelekwe na vifungwe ndani ya muda ili huduma zianze kutolewa.


“Tunakusudia kumuomba Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aje kufungua hospitali hii kabla ya Desemba 30 mwaka huu, hakikisheni vifaa vyote vinaletwa na kufungwa ili Desemba 20 huduma zianze kutolewa kwa wananchi.”


Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Desemba 3 mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliahirisha maadhimisho ya sherehe za miaka 59 Uhuru zilizokuwa  zifanyike Desemba 9, 2020 na kuelekeza kiasi cha shilingi Milioni 835,498,700 zilizotengwa kwa ajili ya sherehe hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru.


Pia Rais Mhe. Magufuli aliagiza vitu vya muhimu kufanyika kupitia fedha hizo ujenzi wa uzio wa kuzunguka eneo la hospitali hiyo pamoja na ujenzi wa barabara ya njia mbili ya kuingilia na kutoka katika hospitali ya Uhuru.


Aidha Mhe. Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhakikisha vifaa vyote vinapatikana haraka ili mkandarasi aweze kukamilisha ujenzi huo na kukabidhi hospitali ili ianze kutoa huduma kwa watanzania.


Mhe. Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa Mkoa na MSD kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha upatikanaji wa vifaa tiba vilivyo katika orodha ya mahitaji ya hospitali hiyo.


“Vifaa vyote ambavyo tumechangiwa na wadau vifikishwe hapa ili kuweza kusambazwa na kufungwa kwa ajili ya kuanza kutumika pale tutakapoanza kutoa huduma”, amesema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Satano Mahenge ameeleza changamoto ya wataalamu wa Sekta ya afya inayokabili Mkoa kwa sasa na ameomba kupatiwa wataalam zaidi.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Rajabu Mabele amesema kuwa vifaa vyote vinavyohitajika vikifikishwa kwa wakati wataweza kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa.


MWISHO

Share To:

msumbanews

Post A Comment: