Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba akiongea na Waandishi wa Habari.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani akiongea na Waandishi wa Habari |
Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika katika Mkoa Singida wakipewa mafunzo.
John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida
Mkoa wa Singida umeandaa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika katika Mkoa ili kuwasaidia kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria huku wakitanguliza mbele maslahi ya wakulima.
Akifungua mafunzo hayo leo mjini Singida kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia eneo la Uchumi Beatus Choaji amesema Mkoa umeamua kufanya mafunzo hayo kutokana na kupata taarifa ya ukaguzi uliofanywa kwenye vyama vya ushirika kushindwa kufanya vizuri.
Choaji amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho kwa viongozi wa Vyama Vya Ushirika na maafisa wengine wa Serikali ambao wamekuwa wakishirikiana na walanguzi kuwanyonya wakulima ambapo amesema hili ni kosa kisheria na kuwaonya kwamba katika kipindi cha sasa Sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwatia hatiani kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi.
“Nawaagiza Watumishi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake fanyeni kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria huku mkitanguliza mbele maslahi ya wakulima”aliongeza Choaji
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba amesema lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kutoa elimu ya kuwawezesha Watendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Nyamba amesema kumekuwa na makosa mbambali ya kiuzembe na kitaaluma katika utendaji wa kazi lakini kupitia mafunzo haya watendaji wote watabadilika.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani amesema pamoja na mambo mengine wajumbe wa kikao hicho watafundishwa masomo ya uandishi wa vitabu vya mwanzo na vitabu vikuu,uaandaaji wa taarifa za fedha,uongozi na utawala pia na Sheria ya Vyama Vya Ushirika Na.6. ya Mwaka 2013
Ameyataja masomo mengine yatakayo fundishwa kuwa ni uandaaji wamakisio ya mapato na matuminzi,uandaaji wa mpango mkakati, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa fedha na udhibiti wa rushwa katika vyama vya ushirika.
Baadhi ya washiriki katika wa mafunzo hayo wamepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Tano kutoa mafunzo na kusema kwamba yataongeza tija katika utendaji wao wa kazi.
Mwenyekiti wa AMCOS wa Wilaya ya Ikungi Mnang’ana Rukia Jumanne amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua majukumu ya kila mmoja kwenye vyama vya ushirika hivyo yatawawezesha kufanya kazi bila kuingiliana nakwa weledi tofauti na kipindi cha awali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kwamba kwa sasa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuufanya Mkoa wa Singida kuwa miongoni mikoa itakayozalisha kwa wingi mazao na kuilisha Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika na dunia kwa ujumla na hivyo kuwa na Vyama vya Ushirika makini ni jambo lisiloepukika kwenye Mkoa wa Singida.
“Tumeanza vizuri kwenye zao la Korosho na Alizeti sasa tunaongeza nguvu kufufua na kuanzisha mazao ya Mkonge na Parachichi” aliongeza Mhe. Nchimbi
Post A Comment: