Na Grace Semfuko, MAELEZO.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amezitaka Taasisi zinazosimamia sekta ya sanaa kuandaa mikakati ya kuboresha na kuendeleza sekta hiyo.
Dkt. Abbasi amesema wasanii wamekuwa wakifanya kazi kubwa na kuingiza mapato katika kazi zao na hivyo ipo haja ya kuweka mfumo mzuri wa ukusanyaji wa mapato ili wafurahie matunda ya kazi zao.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni mpango mkakati wa kuimarisha taasisi hizo.
“Wasanii ni watu muhimu sana na wanafanya kazi kubwa, lakini ni watu ambao wanadhulumiwa sana haki zao, kuna malalamiko makubwa sana wasanii wanaibiwa sana, lazima mamlaka yetu ya kisheria iwalinde wasanii hawa, wananyonywa sana” amesema Dkt Abbasi.
Ameongeza kuwa nia kubwa ya Serikali ni kuhakikisha anapatikana wakala mzoefu aliyethibitishwa katika kazi ya usambazaji wa sanaa zao ili waweze kupata haki kupitia kazi zao.
“Sisi Serikali nia yetu ni kuona anapatikana Mtanzania atakeshughulikia usambazaji wa kazi za wasanii, kazi hii kwa sasa inafanywa na mtu wa nje ambaye anaamua tu namna ya kusambaza kazi hizo, hii ni changamoto kubwa, tunaangalia ni kwa namna gani tunaweza kuitatua” amesema Dk. Abbasi.
Kwa upande wa suala zima la haki miliki Dkt. Abbasi amesema Wizara yake inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha wasanii wanakuwa na haki miliki ya kazi zao ili kuepusha wizi wa sanaa zao.
“Kwenye hati miliki tunahitaji kufanya kitu kikubwa zaidi kuliko tunachofanya sasa, wasanii wanahitaji kuwa na haki katika kazi zao” amebainisha Dkt. Abbasi.
Aidha aliitaka Bodi ya Filamu Tanzania kuwa waratibu wakuu wa shughuli zote zinazohusisha wasanii nchini ili kuondokana na malalamiko ya wasanii kudhulumiwa fedha pindi wanapofanya kazi za sanaa kwenye shughuli mbalimbali za Serikali.
“Kwa upande wa Bodi ya Filamu tunataka nyie ndio muwe waratibu wakuu wa wasanii pindi wanapoitwa kufanya kazi zao, yaani wakija watu wanahitaji wasanii, basi ninyi bodi ya filamu ndio muwe waratibu wakuu kwa sababu kuna wajanja fulani ambao kazi yao ni kuwanyonya wasanii” alisema.
Post A Comment: