Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Aboubakar Kunenge amewaelekeza baadhi ya Wakazi wa eneo la Kunduchi Mtongani ambao nyumba zao zimepitiwa na ujiuji wa volcano ya tope linalofuka kutoka ardhini kuhama Mara moja ili kujikinga na maafa wakati Serikali inaendelea kufanya utafiti wa kujua ukubwa wa eneo lililoathirika.


Mapema leo RC Kunenge akiongozana na wajumbe wa kamati ya usalama ya Mkoa wamefika Katika eneo hilo na kushuhudia uwepo tope linalotoka ardhini na kupanda Katika uso wa ardhi jambo lililosababisha baadhi ya nyumba kutitia, kupasuka nyufa na mifugo kutitia jambo lililosababisha taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.


Kutokana na hali hiyo RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuweka alama za hatari Katika eneo hilo wakati Serikali chini ya taasisi ya Geologia na utafiti wa Madini Tanzania ukiendelea kupia ukubwa wa eneo lililoathirika.


Pamoja na hayo RC Kunenge amesema Serikali inaangalia utaratibu wa kuwapatia wananchi wa eneo hilo Viwanja vingine ili waweze kuendelea na maisha kama awali.


Kwa upande wake Mtafiti kutoka taasisi ya Geologia na utafiti wa Madini Bwana Gabriel Mbogoni amesema matokeo awali wamebaini chanzo Cha tope hilo ni mgandamizo uliosababishwa na uwiano wa maji na chembechembe za udongo kuharibika na kusababisha tope ambalo linasukumwa kutoka chini kwenda kwenye uso wa ardhi.


Aidha Bwana Mbogoni amesisitiza kuwa tope hilo wamelipima na kukuta likiwa na joto la kawaida hivyo halina uhusiano wowote na ile volcano inayorusha majivu na Moto utokanao na miamba iliyoiva hivyo eneo hilo kwa Sasa ni tete na halifai kwa shughuli za Ujenzi Wala makazi.

Share To:

Post A Comment: