NA MWANDISHI WETU, CHALINZE.


MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameanza ziara maalum ya kutembelea  miradi mbalimbali inayoendelea ndani ya jimbo hilo ambapo leo amekutana na wafanyakazi wa DAWASA-Chalinze pamoja na kukagua miradi miwili ikiwemo mradi wa Maji wa Ruvu juu na ule wa CHALIWASA


Katika ziara hiyo, Ridhiwani Kikwete aliweza kutembelea eneo la Chamakweza na Msoga panapofungwa mitambo ya kuongezea msukumo wa maji na kisha kupokea taarifa ya Maendeleo ya Miradi hiyo.


Awali akiwasilisha taarifa hiyo, Meneja wa DAWASA Chalinze, Honest Makoi alisema miradi mikubwa miwili ambayo kwa sasa Wakandarasi wapo kazini wakiendelea na utendaji  inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwaka 2021.


"Tunaishukuru Serikali kwa miradi hii lakini pia tunafarijika kwa ujio wa Mbunge wetu wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete umetuongezea nguvu katika utendaji wetu.


Tuna mradi wa  Kitaifa wa Awamu ya tatu Chalinze ambapo mradi huu mkandarasi wake atafanya upanuzi wa mitambo, upanuzi mfumo wa usambazaji maji na  ujenzi wa vizimba vya maji kwa Wananchi na pia ujenzi wa matenki mbalimbali kwa maeneo yaliyokuwa na matenki ikiwemo yale yalipo maeneo ya Pingo, Pera na Kibiki." Alisema Makoi.


Aidha, Makoi aliutaja Mradi mwingine ni ule wa Mlandizi-Mboga unaotoa maji kutoka Ruvu Juu mpaka eneo la Mboga ambapo utaingiliana na mfumo uliokuwepo ili kuongeza nguvu ya kusukuma maji mpaka Morogoro.


"Miradi hii  inayoendelea italeta mageuzi makubwa sana ya maji, sio maji ya vioski tu hii ni hata maji ya majumbani" Alisema Makoi.


Kwa upande wake, Mbunge, Ridhiwani Kikwete  aliwashukuru DAWASA kwa hatua kubwa wanazoendelea kufanya na kumshukuru Mheshimiwa Raisi Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuwaangalia wananchi wanyonge wa Chalinze kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali ikiwemo za Maji. 


"Mimi kama kiongozi ambaye nimepata dhamana ya kuongoza watu ninachokiona mimi mwenyewe kwakweli nafsi yangu imeniridhisha nina hakika ndoto ya Wananchi wa Chalinze ya maji inaenda kukamilika.


Kwakweli juhudi zinaonekana na pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Meneja na Wafanyakazi wote wa DAWASA kwa kazi nzuri wanayofanya."


"Kwangu mimi ni kuwapa ushirikiano. Kwa sababu wananchi wa Chalinze wanachokitaka ni maji na mimi kama kiongozi wao ni kuhakikisha kwamba ndoto zao zinafikiwa.


...Ili kufikiwa lazima mimi niwape ushirikiano wenzetu wa DAWASA na wao watu ushirikiano kwa maana kiutendaji zaidi." Alisema Ridhiwani Kikwete. 


Ziara ya kutembelea sehemu za huduma za Jamii zinaendelea ambapo pia anatarajia kutembelea Ofisi za TARURA kujua hali ya maandalizi ya marekebisho ya Miundombinu ya barabara vijijini na mijini ndani ya Jimbo hilo.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: