Na Hazla Quire

Imeelezwa kuwa ndugu wa karibu wamekuwa chanzo cha ukatili kwa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti ndani ya familia jambo ambalo liliongezeka kipindi cha likizo ya korona.


Alieleza hayo M/kiti wa shirika linaloshughulika na wanawake na watoto (Save new generation) Bi. Sity Basiali kupitia utafiti uliotokana na mkutano wa zoom ulioandaliwa na Rida Online kwamba ukaribu wa kuleta familia kukaa kwa pamoja kipindi hicho kuliongeza kasi ya ukatili kwa watoto.


Akieleza juu ya utafiti alioufanya alisema kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo watoto walikaa nyumbani ili kuepuka maambukizi ya homa kali ya mapafu korona, walijikuta kwenye hatari zaidi na shirika lake  walilazimika kuelimisha familia zisipeleke watoto kwa ndugu ambao wamekuwa mwiba kwa ukatili. 


"Matukio mengi ya watoto kubakwa au kulawitiwa yanatokana na watu wa karibu ambao wazazi wamewaamini kama wajomba na baba wadogo hivyo tulihakikisha kwa kadri ya uwezo wetu tunazifikia kaya kuelimisha hilo, ambapo nyumba kadhaa tulizozifikia tulikuta tayari baadhi ya watoto wamekumbwa na kadhia hiyo" alisema.


Aliongeza kuwa shule zilifungwa kwa usalama wa watoto lakini kwa wakazi wa mijini ambao wana vyumba vichache vya kuishi watoto walikuwa hatarini zaidi kwani walilazimika kurundikana kwenye chumba kimoja jinsia tofauti au wengine kupelekwa kwa ndugu ambapo hapakuwa salama pia. 


Kwa upande wake Bi. Lilian Liundi ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa jinsia Tanzania TGNP alisema wao walibaini watoto kufanya biashara ikiwemo uuzaji wa barakoa badala ya kukaa nyumbani ambako ndio lengo la kufunga shule ili waepukane na misongamano. 


"Kipindi cha korona tulipishana na watoto wakitembeza chai, wakiuza barakoa, wakichoma mahindi na biashara nyinginezo, wakati dhumuni la likizo ni ili kuhakikisha usalama wao"aliongeza.


Mbali na hilo kulikuwa na ukatili kwa watoto lakini wanafamilia walikaa kimya bila kuwapeleka wahusika kwenye vyombo vya sheria kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya korona iliyokuwa imetanda miongoni mwa jamii achilia mbali kumaliza masuala hayo kindugu.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: