Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na wajumbe wa kamati ya siasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida na wananchi waliojitokeza kumpokea alipowasili kwa ajili ya ziara ya siku moja ya kutembelea nyumba alizokuwa akiishi mkoani humo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha.
Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akipata maelezo katika ziara hiyo. Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha.
Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akisalimiana Mzee Andrew ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi wakati akifanyakazi mkoani Singida.
Na Mwandishi Wetu, Singida
RAIS mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekanusha taarifa zilizopo Mkoani Singida kwamba kiwanja alichopewa kwa ajili ya makazi amekiuza kwa moja ya waumini wa makanisa yaliyopo mjini Singida.
Dkt. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Taifa, alitoa kauli hiyo mjini Singida alipokuwa katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea na kukagua nyumba alizowahi kuishi zaidi ya miaka 40 iliyopita wakati akiwa mtumishi wa chama cha TANU.
Alifafanua kiongozi huyo mstaafu kwamba mwaka 1975 akiwa Katibu Msaidizi wa Chama Cha TANU aliishi katika nyumba tano tofauti tofauti kabla na baada ya kwenda jeshini kwa hali hiyo anazifahamu kikamilifu mali za chama mkoani Singida zilipo.
“Kiwanja changu sijampa mtu yeyote yule kama wamechukua kanisa waulizeni,kama ni kiwanja changu waulize,kama ni kiwanja changu tulipatana wapi mimi na wao? alihoji raisi huyo mstaafu.
Akizungumzia moja ya nyumba alizowahi kuishi wakati akiwa mtumishi wa chama katika kipindi hicho,Dkt. Kikwete alisisitiza kwamba nyumba ile alikuwa akiishi baada ya kurejea kutoka jeshini.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu alisema baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa rais na mwenyekiti mstaafu wa CCM, Dkt Jakaya Kikwete watayafuatilia ili waweze kujua ukweli kuhusu kiwanja alichokuwa amepewa kiongozi huyo mkuu ya nchi.
“Tumepokea maelekezo na tutayafuatilia na kwa bahati nzuri na kamisaa wetu DC alikuwepo anasikia kwamba kuna kiwanja cha Mheshimiwa rais mstaafu Jakaya Kikwete eneo la Somoku tutafuatilie vile vile hapo alipokuwa akikaa zamani ambako amesema ilikuwa nyumba ya TANU tutaifuatilia na tutatoia matokeo yake.”alisisitiza Kaburu.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha amemuhakikishia Mwenyekiti huyo mstaafu wa chama hicho Dkt.Jakaya Kikwete kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa CCM wa mkoa huo watahakikisha moja ya nyumba mali ya TANU aliyokuwa akiishi wakati akifanyakazi mkoani hapa umiliki wake unarudishwa kwenye CCM kwani hivi sasa anaishi mfanyabiashara mmoja.
"Sisi kama vijana wa CCM kwa kushirikiana na viongozi wetu tutafanya uchunguzi ili kujua mfanyabiashara huyo alipateje nyumba hiyo iliyokuwa mali ya TANU na sasa CCM" alisema Nyiraha.
Post A Comment: