Na Shamimu Nyaki-WHUSM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi
ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini kukutana na Wadau wa sekta hiyo
wakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa namna
ya kuendesha michezo kwa pamoja na kutoa ushauri wa kisera kwa wadau hao.
Dkt. Abbasi ametoa maagizo hayo leo Novemba 21, 2020 Jijini Dodoma katika kikao
watumishi wa Idara hiyo ambapo amewataka kusimamia kikamilifu Sekta ya Michezo
ambayo inaendelea kuletea heshima Taifa.
"Ni lazima mkutane na Wadau wenu ili mjue wana mawazo gani katika sekta hii na nyie
mtoe ushauri wa kitaalamu ambao utaleta tija. Ni lazima muwaeleze wadau Sera ya
Michezo inasemaje kwa sababu nyie ndio mnaoisimamia sekta hii ", alisema Dkt.
Abbasi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameitaka Idara hiyo kuhakikisha kila Shirikisho au Chama cha
michezo vinawasilisha Mpango Mkakati wake katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
ambao pamoja na mambo mengine, utaonyesha kalenda ya mwaka katika ligi za kitaifa,
kimataifa pamoja na timu ya Taifa . Lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na uelewa
wa pamoja kwa wadau wote utakaoleta mafanikio zaidi katika sekta hiyo.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Taifa lazima liwe na ushiriki wa mashindano ya michezo
ambao utaleta tija, hivyo Idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha mashindano yote ambayo
nchi inashiriki katika ngazi mbalimbali yanakua na manufaa, ameongeza kuwa katika
mashindano mbalimbali ikiwemo Olympiki lazima kama nchi kujua aina ya michezo ya
kushiriki.
Vilevile, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA
ni mashindano ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanazalisha vipaji
vingi vya michezo mbalimbali nchini. Hivyo, Idara ya Michezo ina jukumu la kusimamia
mashindano hayo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo TAMISEMI na Wizara
ya Elimu ili vijana wanaofanya vizuri waendelezwe kupitia Chuo cha Maendeleo ya
Michezo Malya pamoja na sehemu nyingine.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania
Bara na Zanzibar katika sekta ya Michezo unaendelea kuimarika ikiwemo kuimarisha
Kombe la Mapinduzi.
;Muungano wetu ni muhimu na Kombe la Mapinduzi ni moja ya njia ya kutuunganisha
na kuimarisha Muungano wetu, hivyo nitoe rai kwa Vilabu kupeleka timu bora katika
mashindano hayo"alisema Dkt.Abbasi.
Akiongelea kuhusu miuondombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja, Dkt. Abbasi
ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza na matarajio ni kuwa na viwanja bora vya
michezo nchini na tayari Ujenzi wa Uwanja wa Dodoma umefikia hatua nzuri.
Post A Comment: