Mgombea Urais kupitia ADC, Queen Sendiga akihutubia mamia ya wananchi wa Singida Mjini, waliofika kumsikiliza kwenye uwanja wa stendi ya zamani jana.
Queen Sendiga akionyesha mfano wa Karatasi ya Kupigia Kura na sehemu kilipo chama chake na jina lake, ili kuwarahisishia wapiga kura kumtambua kirahisi na kumchagua ifikapo Oktoba 28 .
wa Singida mjini wakisikiliza Sera na Ilani ya ADC kupitia mgombea wake wa nafasi ya Rais.
Wananchi wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
Queen Sendiga akizungumza kwenye mkutano huo.

Wananchi wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
Mkutano ukiendelea.


Na Mwandishi Wetu, Singida

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Madam Queen Sendiga, amesema anaomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Rais wa kwanza mwanamke, lengo hasa ni kutatua kero sugu hususani kwenye la afya, maji, elimu na ajira ambazo zimeshindwa kutatuliwa na mamlaka zilizopo kwa takribani miaka 59 tangu uhuru.  

Sendiga aliyasema hayo, wakati akinadi Sera na Ilani ya ADC kwenye mkutano wa Kampeni za kuwania nafasi ya Rais kwa mwaka 2020, alipohutubia mamia ya wananchi waliokusanyika viwanja vya stendi ya zamani mkoani hapa jana.

“Nimesukumwa kwa dhati ya moyo wangu kama mwanamke…na kama mama kulitumikia Taifa hili kwa nafasi ya Rais, kwa sababu CCM kwa miaka 59 tangu tupate Uhuru imeshindwa kufanya mageuzi stahiki kwa mtanzania katika muktadha wa kimaendeleo licha ya kujaliwa rasilimali zote muhimu,” alisema.

Alisema kitendo cha yeye kutokata tamaa, licha ya idadi ya wagombea hai wa kinyanganyiro cha nafasi ya Rais toka 15 mpaka kubakia wanne kwa sasa, ni dalili tosha na kiashiria cha wazi kwamba ana mapenzi ya dhati-na ya ‘kimama’ ya kutaka kulitumikia Taifa kwa upendo na matarajio chanya kwa kila mwananchi.

Akizungumzia sekta ya afya alisema suala la bima kwa kila mwananchi bila ya masharti yoyote halikwepeki, na kwamba nchi zote zilizoendelea zimewekeza na kutoa msukumo kwenye huduma za afya kwa kuamini kwamba huduma bora za afya ndio msingi wa ustawi wa afya ya raia kwa matokeo chanya ya mageuzi ya kiuchumi.

Aidha, katika elimu mwanamke huyo ambaye kama atapewa ridhaa na watanzania atakuwa Rais wa kwanza Mwanamke tangu Uhuru na wa 3 kwa Bara la Afrika, alisema anaamini maisha duni ni matokeo ya elimu duni.

“Elimu ni kila kitu, elimu ndio ufunguo wa maisha. Mtu akikunyima elimu bora ujue amekunyima maisha, tusisahau pia ndugu zangu elimu bora sambamba na maarifa yenye tija, ni matokeo chanya ya umahiri na ufanisi kwenye taaluma nyingine mbalimbali,” alisisitiza Sendiga.

Katika suala la elimu, alisema ADC kwanza watahakikisha wanatoa elimu bure kweli kweli, pia watajikita katika kutoa maarifa na sio kukaririsha kama ilivyo kwa sasa, na zaidi watabadili mtaala uliopo ili kumfanya mwanafunzi afundishwe ‘elimu maarifa’ kwa kuzingatia elimu bila maarifa ni kazi bure.

Hata hivyo, Sendiga akizungumzia suala la ajira, alisema mkakati wa chama hicho chini ya serikali yake ni kuhakikisha wanakwenda kuzalisha ajira milioni 10, kwa kuhakikisha wanatengeneza miundombinu rafiki kwenye sekta zote mtambuka, ikiwemo kilimo, uvuvi, elimu maarifa na nyinginezo.

“Chama chetu kitashughulikia kwa nguvu zote changamoto zote zilizopo sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwepo na pembejeo za kutosha, masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, maboresho ya miundombinu kwenye sekta mbalimbali vijijini, ikiwemo maji safi na salama, na ubora wa elimu,” alisema.

Katika kuthibitisha hali ya ukomavu wa kisiasa, uzalendo wa kipekee na nia yake ya dhati ya kuendelea kuwa miongoni mwa wapigania maslahi ya amani ya Tanzania, kama jina lake lilivyo maarufu “Mama wa Taifa” Sendiga aliwasihi wananchi kuhakikisha ifikapo Oktoba 28 wakichapiga kura ya kumchagua yeye na wabunge wa chama chake basi warudi nyumbani kusubiri matokeo.

“Ukipiga kura rudi nyumbani..tunza amani. Ukifanya vurugu yoyote utakamatwa na kushtakiwa kwa jinai kama mhalifu mwingine yeyote na utajikuta ukiishia kuozea jela. Hutahukumiwa kama mwanachama wa chama fulani bali kama mhalifu,” alionya Sendiga, ambaye Singida ni mkoa wake wa 16, tangu aanze kampeni hizo.

Share To:

Post A Comment: