Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) akipokea cheti cha hati ya ushindi wa nafasi ya ubunge kutoka kwa Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Simanjiro Yefred Myenzi baada ya kumtangaza kushinda nafasi hiyo.
Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) akionyesha cheti cha hati ya ushindi wa nafasi ya ubunge baada ya kumtangazwa kushinda nafasi hiyo.
Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) akionyesha cheti cha hati ya ushindi wa nafasi ya ubunge baada ya kumtangazwa kushinda nafasi hiyo, kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Awadhi Omari, Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri hiyo Jackson Sipitieck na Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo Ally Kidunda.

Mbunge mteule wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) akiwashukuru wananchi wa Kata ya Edonyongijape baada ya kutangazwa kushinda ubunge wa jimbo hilo.



 Na Gift Thadey, Simanjiro


MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) ameibuka kidedea na kwa kupata kura 54,609 na kumgaragaza mgombea wa Chadema Emmanuel Ole Landey aliyepata kura 8,782. 

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro, Yefred Myenzi akitangaza matokeo hayo mji mdogo wa Orkesumet amesema wapiga kura waliojiandikisha ni 133,086. 

Myenzi amesema kati ya hao waliojiandikisha, waliopiga kura ni 64,238 na kura halali ni 63,391 na kura zilizokataliwa ni 847. 

Amesema kwa upande wa wagombea udiwani, CCM imepata kata zote 18 kwani awali wagombea nane walipita bila kupingwa hivyo ikashinda kwenye kata 10 kulikokuwa na wagombea wa Chadema. 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi wa nafasi hiyo, mbunge mteule wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka aliwashukuru wananchi wote kwa kumpatia fursa hiyo ya kuwa mwakilishi wao Bungeni. 

``Imani huzaa imani, ninawaahidi kuwapa utumishi uliotukuka sawa sawa na dhamira yenu ya dhati mliyonipa kwa kunichagua kwa kura nyingi takribani asilimia tisini hivyo baada ya kuapishwa nitaanza kuwatumikia kikamilifu japokuwa nimeanza kabla ya kuapishwa,`` amesema Ole Sendeka. 

Amewashukuru wananchi wa jimbo la Simanjiro kwa kumpatia kura nyingi za kishindo mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho Dk John Pombe Magufuli kwani wametekeleza ahadi yao kuwa watampa kura nyingi za ndiyo. 

``Mgombea urais wa CCM Dk Magufuli ameongoza kwenye vituo vyote katika kata zote 18 za Jimbo la Simanjiro kuanzia Mirerani, Naisinyai, Orkesumet, Naberera , Ojloro Namba tano, Edonyongijape, Ngorika, Msitu wa Tembo, kila mahali,`` amesema Ole Sendeka. 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jackson Leskari Sipitieck (CCM) alishinda nafasi ya udiwani wa Kata ya Langay kwa kupata kura 1,929 dhidi ya mgombea wa Chadema Saning`o Abel aliyepata kura 329. 

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Orkesumet Edmund Tibiita alimtangaza aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Sendeu Laizer Obama wa CCM kuwa alishinda udiwani Kata ya Orkesumet kwa kupata kura 1,076 dhidi ya Mwenda Sikapesia wa Chadema aliyepata kura 837. 

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Endiamtu Charles Msangya amesema mgombea udiwani wa Kata ya Endiamtu kwa tiketi ya CCM, Lucas Zacharia Chimbason Agwiso alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 3,265 hivyo kumbwaga aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya Chadema Philemon Oyogo aliyepata kura 816. 

Madiwani wateule wa CCM waliopita bila kupingwa ni Salome Mnyawi (Mirerani), Jackson Ole Matery (Terrat), Ezekiel Lesenga Mardad (Loiborsiret) Lesakwi (Oljoro namba tano), Taiko Kurian Laizer (Naisinyai) Julius Lendauwo Mamasita (Shambarai) Yohana Shinini (Emboreet) na Baraka Kanunga (Komolo).
Share To:

Post A Comment: