Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametoa maelekezo kwa wanaCCM wote nchini, kufunga kampeni saa tisa alasiri, ili kutoa muda kwa wanachama na wananchi wote kumsikiliza Mgombea Urais wa CCM Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuanzia saa kumi alasiri tarehe 27 Oktoba, 2020 atakapokuwa akizungumza kupitia vyombo vya habari katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convetion Center Jijini Dodoma.
Ameyasema hayo leo tarehe 24 Oktoba, 2020 wilayani Babati katika kikao cha mawakala wa CCM na viongozi mbalimbali wa Mashina, matawi, Kata, wilaya na mkoa.
"Kamati zote za ushindi wanaelekezwa na Mwenyekiti na Mgombea wetu wa Urais waendelee na kampeni bila kuchoka mpaka saa tisa alasiri tarehe 27 Oktoba. Saa kumi alasiri Mwenyekiti, Rais wetu na Mgombea wetu Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atahutubia wanachama na wananchi wote akiwa Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, na hotuba hiyo yenye ujumbe mahususi ataitoa kupitia vyombo vyoote vya habari na itakuwa mubashara"
Aidha Katibu Mkuu, ametoa maelekezo kuwa wagombea wote wakiwemo waliopita bila kupingwa ngazi za Udiwani na Ubunge, kufanya mikutano mfululizo kuanzia sasa na siku ya tarehe 27 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa tisa alasiri, wagombea wote wakiwemo waliopita bila kupingwa ni lazima wawe wamefanya mikutano ya kuhitimisha kampeni kabla ya kuanza kumsikiliza Mgombea wa Urais saa kumi alasiri.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo, kutoa elimu kwa wapiga kura ambapo amewataka wanachama wote siku ya tarehe 28 kutokuvaa sare za Chama, na kwa wale waliopoteza shahada zao za kupigia kura wanaweza kutumia Vitambulisho vya NIDA, leseni ya udereva na hati ya kusafiria.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu amewahakikishia wanachama na wananchi wote, kuwepo na usalama wa kutosha siku ya kupiga kura na kutangazwa matokeo, hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya tarehe 28 Oktoba, 2020, baada ya kupiga kura kurudi na kusubiri mamlaka zinazohusika kutangaza matokeo.
Kesho tarehe 25 Oktoba, 2020, Katibu Mkuu baada ya mkutano wa Kampeni wa Mgombea Urais wa CCM, ataweka jiwe la msingi katika ujenzi unaoendelea wa Ofisi za CCM mkoa wa Manyara.
Kikao hiko kimehudhuriwa na viongozi mbalimabli wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara Ndg. Saimon Lulu
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Afisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Post A Comment: