Na Mwandishi Wetu,
KATIKA kuhakikisha inapata watalaamu mbalimbali wa kuendesha ajenda zao,Jumuiya ya Afrika Mashariki imesaini makubaliano maalum na Serikali ya Ufaransa ya kuanzisha mfumo na mkakati wa kupata watalaamu hao ili kuhakikisha shughuli za maendeleo zinaendelea kuimarika kwa nchi zilizopo kwenye jumuiya hiyo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inaeleza kwamba makubaliano hayo yamesainiwa jijini Arusha katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC baina ya Balozi wa Ufaransa, Fredrick Clavier na Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko.
Makubaliano ya pande hizo mbili yamelenga maeneo makuu matano ambayo pande hizo mbili zimepanga kuona matokeo ambayo ni nishati, mabadiliko ya tabia nchi, viwanda, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji huduma na biashara, sekta ya fedha na kuwajengea uwezo katika miradi ya maendeleo.
Akizungumzia makubaliano yao, Balozi Clavier amesema wamejadiliana kwa kina na EAC namna pande hizo zitakavyofanya kazi katika kuzilinda sekta muhimu na kuinua maisha ya watu.
" Katika miaka 10 iliyopita kiasi cha fedha kilichotengwa AFD kiliongezeka kutoka euro milioni 31 hadi 172 kwa miradi ya sekta ya maji na usafi wa mazingira, nishati, afya na hasa miradi ya maji na usafi wa mazingira wa ziwa Viktoria uliogharimu euro milioni 76," Amesema Clavier.
Amesema katika makubaliano hayo, mkakati mwingine ni kuhakikisha wadau muhimu wa maendeleo na nyanja nyingine za kijamii kuwa pamoja kwa maslahi ya jukuiya na katika hilo ubalozi wa Ufaransa nchini umeeleza wazi ambavyo umedhamiria kushirikiana na jumuiya hiyo.
"Mkubaliano haha yanafungua ukurasa mwingine wa ushirikiano kati ya Serikali ya Ufaransa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa muda mrefu tumekuwa na ushirikiano nzuri na sasa kusainiwa kwa makubaliano hayanaa tunakwenda kuimarisha zaidi hasa maeneo ambayo tumeyalenga ndani ya makubaliano tuliyoingia,"amesema.
Katibu Mkuu wa EAC Balozi Mfumukeko ameishukuru serikali ya Ufaransa kwa kukubali ushirikiano katika jitihada mbalimbali za kuinua maendeleo kwenye sekta mbalimbali kwa ukanda wa Afrika Mashariki."Makubliano haya ambayo tumesaini ya Serikali ya Ufaransa kwetu yamekuja wakati sahihi sana.Ni matumaini yetu tunakwenda kupiga hatua zaidi kwa jumuiya yetu katika nyanja mbalimbali na kuleta maendeleo yetu."
Matukio ya picha mbalimbali wakati wa tukio hilo la utiwaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Ufaransa na Jumuiya ya Afrika Mashariki
Post A Comment: