Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu akizungumza, kushoto (aliyevaa miwani) ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda.
Mratibu wa zao la Korosho kitaifa, Dk Geradina Mzena akizungumza na wanahabari wilaya ya Manyoni.
Kikundi cha Food and Drinks (FND) kutoka Dar es Salaam kikishiriki mafunzo hayo kwenye shamba la Masigati.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida
KASI ya Mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho yanayoendelea kutolewa kwa mafanikio makubwa na Kituo mahiri cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Naliendele kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho, pamoja na programu ya uanzishaji wa mashamba makubwa ‘Block Farming’ likiwemo shamba la Masigati Wilaya ya Manyoni mkoani hapa, vipo kwenye Ibara ya 37 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu aliyasema hayo eneo la Masigati jana wakati akishiriki sehemu ya mafunzo kwa vitendo yanayoendelea kutolewa na kituo hicho kwa wakulima na maafisa ugani wa mikoa 17 nchini, ikiwemo Morogoro, Dodoma na Singida
“Ukienda kwenye ilani ya CCM ibara ile ya 37 tumeelekezwa kuhakikisha tunaanzisha mashamba makubwa ya mazao ya kimkakati na kutoa huduma za kiugani. Kwahiyo ‘block farming’ hizi mnazoziona hapa Manyoni ni mkakati wa serikali katika kutekeleza ilani, lengo hasa ni kuongeza tija na uzalishaji” alisema Chimagu
Alisema Tanzania bado inakabiliwa na ushindani mkubwa kwenye eneo la uzalishaji kukidhi mahitaji ya soko la korosho ikitanguliwa na nchi za Vietnam, India, Brazil na Ivory Coast, ambapo mpaka sasa kiwango cha uzalishaji kama taifa kimefikia tani laki 315 huku shabaha iliyopo ni kufikia tani milioni moja ifikapo 2023
Chimagu alisema mkakati wa serikali uliopo ni kupanua wigo wa uanzishaji viwanda vya ndani vya zao hilo ili kukuza uchumi wa zao hilo kwa kuliongezea thamani tofauti na ilivyo sasa, lakini vitafungua milango ya ajira na kuimarisha vipato vya wakulima, huku akibainisha uchache wa viwanda hivyo kwa sasa ambavyo uwezo wake ni kuchukua tani 175 pekee, huku tani nyingine ghafi zikiuzwa nje
“Sisi tuna faida korosho yetu ni nzuri na ni bora sana. Ina soko kubwa na la uhakika hasa Vietnam na India, niwasihi watanzania changamkieni fursa hii kwa kuanzisha mashamba mapya. Bado kuna maeneo ya kutosha ya kulima zao hili..na kwa wale wanaoongeza mashamba endeleeni kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo na msisahau kutumia mbegu bora za serikali kutoka pale Tari Naliendele,” alisema
FAIDA ZA MASHAMBA
MAKUBWA (BLOCK FARMING)
Chimagu alisema kupitia kilimo cha mashamba makubwa wakulima eneo hilo kwa pamoja wanapata fursa ya kupata mafunzo ya nadharia na vitendo kwa urahisi zaidi kuanzia kwenye uandaaji wa shamba, namna ya kulihudumia, uvunaji wake na hatimaye kupata mavuno bora yanayokidhi viwango vya masoko ndani na nje ya nchi
Faida nyingine kunakuwa na utaratibu wa kupata pembejeo kwa pamoja sambamba na kuwa na uhakika wa takwimu. Mathalani shamba la masigati pale manyoni lina jumla ya ekari elfu 22, ambazo ni rahisi kuweza kuwa na makadirio ya uhakika ya kiwango cha uzalishaji kinachostahili.
Pia wakulima wakiwa eneo moja ni rahisi sana kufikisha huduma za viuatilifu na pembejeo kwa wakati, lakini hata kudhibiti upandaji wa miche kwa idadi inayotakiwa. Kwa mfano ekari moja ya korosho inahitaji miche 27, lakini unakuta maeneo mengine idadi hiyo inakuwa chini au zaidi ya kiwango kinachotakiwa
Chimagu alisema hata wakati wa mavuno uvunaji unafanyika kwa wakati mmoja ili kuweza kukidhi masoko yanayotakiwa. Aidha alisema korosho ni rafiki wa mazingira, mathalani kipindi hiki ni kiangazi lakini kwa mujibu wa Chimagu ukitembelea shamba lililopo Masigati utakuta rangi ya kijani imetamalaki
“Niwasihi watanzania waje kujifunza kupitia mashamba haya makubwa yaliyopo eneo la Masigati hapa Manyoni na Dodoma ili wapate hamasa ya kuzalisha kwa ubora, na hatimaye malengo yetu ya tani laki na elfu kumi na tano kwenda milioni moja miaka mitatu ijayo yaweze kufikiwa,” alisema Chimagu.
Post A Comment: