Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dodoma baada ya kuhitimisha kampeni zake za uchaguzi 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Hassan Kilimba akiwa katika moja ya mikutano ya kampeni Tarafa ya Makiungu mkoani hapa. 


Na Godwin Myovela, Singida


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa Alhaji Juma Hassan Kilimba amesema kwa idadi ya kura zote zitakazopigwa kwa nafasi ya Udiwani, Ubunge na Rais, chama hicho kinatarajia kuibuka na ushindi wa asilimia 83.75

Akitoa ufafanuzi mbele ya vyombo vya habari jana, Kilimba alisema kwa kuanza na madiwani CCM ilisimamisha viti vyote 136, na kati ya hivyo viti 35 vilipita bila kupingwa hatua iliyokifanya chama hicho kubaki kikishindania viti 101 vya nafasi hiyo pekee.

Kilimba alisema kwa upande wa Ubunge walifanikiwa kusimamisha wagombea wote 8 kwa idadi ya majimbo yaliyopo, na katika siku zote 60 za Kampeni, kuanzia Septemba walipoanza mpaka sasa wamemaliza salama, hakukuwa na tatizo lolote.

Kada huyo wa CCM alisema katika kipindi chote cha kampeni walifanikiwa kuwa na mikutano mikubwa ya kitaifa 34, ambapo kati yake mgombea wa nafasi ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli alikuja mkoa wa Singida na kufanya mikutano ya hadhara 7, huku Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan akifanya mikutano ya hadhara mitano.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu alifanya mikutano ya hadhara 3, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye mkutano 1, Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mikutano 4, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mlezi wa CCM Mkoa Munde Tambwe mikutano 4.

Wengine ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk Bashiru Ally mikutano 8, na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Hery James mikutano 2, idadi iliyopelekea jumla ya mikutano yote ya viongozi wa kitaifa kufikia 34, idadi ya mikutano ya wabunge 8,050, huku Mwenyekiti pamoja na Kamati yake ya Siasa ya Mkoa wakifanya jumla ya mikutano ya hadhara 217.

Kilimba akizungumzia takwimu za awali za stratejia za ushindi kwa upande wa Madiwani, alisema katika kata 136 zilizopo ndani ya mkoa wa Singida…madiwani wamefanikiwa kufanya mikutano ya hadhara 560, idadi ambayo ikijumlishwa na ile mikutano ya ndani kimkoa jumla yake kuu inafikia mikutano 13,520.

Alhaji Kilimba akitoa tathmini hiyo alisema baada ya juhudi kubwa za kampeni kufanyika, ikiwemo mabalozi, madiwani na wabunge kutumia njia ya ‘nyumba kwa nyumba’ hatimaye chama hicho kimeweza kufanikiwa kuifikia idadi yote ya watu 36, 300 mkoani hapa waliojiandikisha kupiga kura.

Kulingana na vyanzo vilivyopo kutoka CCM Singida na Tume ya Uchaguzi, mpaka sasa idadi ya waliojiandikisha mkoani hapa imefikia 848, 833, huku idadi ya wanaotarajia kupiga kura ikifikia laki 7, 44,762.

“Sasa ukitazama mkoa wetu wa Singida tuna wanachama wa CCM laki tatu, arobaini na mbili elfu, mia tano sabini na saba (3,42,577) ambao ni zaidi ya nusu ya wapiga kura wote…” alisema Kilimba.

Hata hivyo, aliongeza kwamba kupitia mikutano hiyo ambayo tulifanikiwa kunadi sera na Ilani yetu kwa Mama Ntilie, Machinga, Waendesha Bajaji na Bodaboda, Vijana, Wazee, Wenye Ulemavu na Wachimba Madini, CCM mkoani hapa mpaka kumalizika kwa ngwe ya mbio hizo za uchaguzi 2020, imeweza kuwafikia wapiga kura zaidi ya milioni 1, yaani (1, 234,540).

 “Matarajio kwa ushindi wa ujumla, kura za Rais tutakuwa na uhakika wa kupata asilimia 92.5, ubunge kwa wagombea wote asilimia 100, na Madiwani asilimia 94.375….lakini kwa idadi ya kura zote baada ya kujumlishwa CCM Singida tutakuwa na asilimia 83.75,” alisema Kilimba.

Share To:

Post A Comment: