Na John Walter-Manyara                                    


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  wilayani Kiteto mkoa wa Manyara, inawashikilia  Daktari Martin John Kongora na Mtaalamu wa dawa za Usingizi Fabian Aweda wa Hospitali ya wilaya ya Kiteto kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa kwa mzee wa Miaka 60.
Takukuru inatambua kosa hilo ni  Kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. 
Akizungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Holle Makungu, amesema wawili hao wanatuhumiwa kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi laki 180,000  toka kwa mzee huyo (jina tunalihifadhi) aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume ambapo waliomba rushwa hiyo ili waweze kumfanyia upasuaji liicha ya kuwa mzee huyo alikuwa na Bima ya Afya iijulikanayo kama ICHF.
Makungu ameeleza kuwa Takukuru wilayani Kiteto ilipokea malalamiko hayo ndipo walipomwelekeza mlalamikaji akawaombe wamfanyie upasuaji  kwa kuwa ana bima ya afya lakini watuhumiwa walikataa na kumwambia endapo ataendelea kubisha wataandika taarifa  kuwa ugonjwa huo hawawezi kuutibu na kwamba watamwandikia rufaa ya kwenda Dodoma ambapo angeingia gharama kubwa zaidi ya malazi na usafiri.
Taarifa ya mkuu wa Takukuru Manyara Holle Makungu imeendelea kueleza kuwa , kwa kuwa Kongora alikuwa mtaalamu pekee katika hospitali hiyo  kwa tatizo hilo na kwamba hali ya mgonjwa iliendelea kuwa mbaya, walielekeza rushwa hiyo wapewe wataalamu hao wa afya wakati ushahidi wa kuomba na kupokea rushwa ukiendelea kukusanywa.
Makungu amesema waliacha mgonjwa afanyiwe upasuaji ambapo waliufanya kwa ufanisi  huku wakisubiri mgonjwa apone na kuruhusiwa kutoka hospitali ndipo walipowakamata  na wanatarajia kuwafikisha mahakamani siku ya Jumatatu Septemba 14 mwaka huu.
Hata hivyo Takukuru mkoani Manyara inakemea kwa nguvu watumishi wachache wa wizara ya Afya wanaokiuka maadili ya Taaluma yao na kujihusisha na vitendo vya rushwa, na wataendelea kuwachukulia hatua za Kisheria.
Aidha Takukuru imetoa Rai kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa bila woga kwa kuwa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 ina Vifungu viinavyowalinda wanaotoa taarifa kwa nia njema.
Share To:

Post A Comment: