Na Ferdinand Shayo ,Arusha.
Walemavu Wilayani Monduli Mkoani Arusha wamepatiwa elimu ya mpiga kura itakayowawezesha kushiriki vyema katika zoezi la kupiga kura Octoba 28 mwaka huu na pia kutambua vipaumbele walivyopewa na tume ya uchaguzi pindi wanapofika katika vituo vya kupigia kura.
Akizungumza na Makundi ya Walemavu Wilayani Monduli ,Mkurugenzi wa Shirika la Okoa New Generation ,Neema Robert alisema kuwa wameamua kutoa elimu hiyo ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua kiongozi wanayemtaka atakayepigania maslahi yao.
Neema alisema kuwa kundi hilo muhimu linahitaji kupata elimu ya mpiga kura na kuhamasishwa umuhimu wa kushiriki katika zoezi la uchaguzi .
“Tume imetoa kipaumbele cha kuwahudumia mapema walemavu ,wajawazito pamoja na wazee hii inaonyesha jinsi gani makundi haya yanapata fursa za kupiga kura bila usumbufu huku wakizingatia sharia za uchaguzi” Alisema Mkurugenzi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Wilaya ya Monduli (SHIVYAWATA) Dorah Christopher amepongeza asasi za kiraia kwa kutumiza wajibu wa kutoa elimu ya Mpiga kura hususan kwa walemavu kundi ambalo limekua likisahaulika mara kwa mara .
Kwa upande wao walemavu Pendaeli Solomon na Godwin Ernest walioshiriki katika kupatiwa elimu ya wapiga kura walisema kuwa elimu hiyo itawasaidia kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi bora na kuyaomba mashirika kufika vijijini na wilaya za pembezoni ili kuwafikia walemavu wengi zaidi.
Post A Comment: