Maafisa Ugani na Wakulima wakifuatilia mafunzo hayo.
Mmoja wa wakulima akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Kaimu Afisa Kilimo Halmashauri ya Bahi, Hamis Mfuko akishiriki mafunzo hayo.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Chamwino
WAKULIMA wa zao la Korosho wamehimizwa kuendelea kutumia aina 54 za mbegu bora za zao la korosho zinazozalishwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele, ambazo zimethibitishwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mavuno yake kwa wingi, sambamba na kuvumilia magonjwa na visumbufu vya wadudu hatarishi wa zao hilo.
Pia imeelezwa kuwa matokeo ya mbegu hizo hata baada ya mavuno hususani kwenye eneo la usindikaji mpaka sasa zimeendelea kutoa matokeo chanya kwenye uzalishaji wa bidhaa zake katika Nyanja ya usindikaji hususani kupitia ‘bibo’ lake kwa kuonyesha ufanisi wa hali ya juu kwa matumizi ya utengenezaji juice, ‘ethanol’ na mvinyo.
Akizungumza na vyombo vya habari, muda mfupi baada ya kutoa mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima kwenye wilaya za Mpwapwa na Chamwino jana, Mratibu wa zao la Korosho nchini kutoka Tari Naliendele, Dk Geradina Mzena alisema endapo mkulima atatumia walau aina zaidi ya 27 ya mbegu hizo basi atakuwa amejihakikishia usalama na uhakika wa mavuno.
Akifafanua, alisema aina hizo 54 ndani yake zimegawanyika katika makundi 3, yaani kuna mbegu 16 ambazo ni za kawaida (kwa maana ya zisizo chotara), pia kuna mbegu 22 ambazo ni chotara, na nyingine 16 ni aina ya mbegu fupi.
Alisema kituo hicho kinatoa mchanganyiko wa makundi ya mbegu hizo zilizofanyiwa utafiti wa kina lengo likiwa ni kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa mkulima, ikiwemo kulikinga zao hilo dhidi ya mashambulizi ya wadudu na magonjwa, sambamba na kumsaidia mkulima kukabili changamoto za kupoteza miche na kujikuta akipata hasara endapo atapanda aina moja ya mbegu katika shamba moja.
“Aina zote hizi kwenye makundi haya matatu ni mbegu bora. Ubora wa mbegu hizi kwanza zina uwezo wa kutoa korosho kubwa, lakini pia zinavumilia magonjwa na zinaota na kuzaa vizuri sana kwenye maeneo yote ndani ya mikoa 17 tuliyoifanyia utafiti,” alisema Mzena.
Alisema mbegu hizo zina uwezo mkubwa wa kuvumilia wadudu waharibifu, na zaidi hata inapojitokeza hali ya mabadiliko ya hali ya hewa zinaendelea kuwa imara na kutoa mavuno yaliyo bora ikilinganishwa na zile za kienyeji.
Zaidi Mzena alisema kupitia aina hizo za mbegu zitamwezesha mkulima kuvuna korosho karanga zenye punje kubwa, ambazo idadi yake inaweza kuwa chini ya 200 kwa kilo moja na hivyo kuleta tija kwa ustawi wa uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kuhusiana na bibo bora linalotokana na aina hizo za mbegu, Mratibu huyo, ambaye pia ni Mtafiti na Mratibu wa Ubunifu kutoka Tari Naliendele alisema kituo hicho baada ya kubaini kuwa bibo linaweza kukaa kwa kati ya masaa 12 hadi 24 kabla ya kuharibika waliamua kuja na teknolojia ya kulikausha na kisha kulitumia kutengeneza aina hizo za vinywaji na bidhaa za vimiminika.
“Kuanzia msimu ujao tunategemea wakulima watakuwa na misimu miwili ya kuuza korosho zao, kwanza watapata fursa ya kuuza korosho karanga, na msimu mwingine watauza bibo la korosho karanga lililokaushwa na hivyo kuzidi kuongeza thamani ya zao hilo,” alisema Mzena.
Post A Comment: