Na Amiri Kilagalila,Njombe
Njombe. Mgombea Ubunge Jimbo la Makete Kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Ahadi Mtweve amesema endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo atahakikisha anatoa bima ya afya bure kwa wazee yenye hadhi sawa na ya mtumishi wa serikali.
Mtweve amesema hayo wakati akinadi sera za chama hicho kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi zilizofanyika kata ya Isapulano wilayani Makete mkoani Njombe .
Amesema iwapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha wazee wenye Umri wa miaka 60 na kuendelea katika jimbo la hilo wanapata matibabu bure kupitia bima atakazowakatia.
Amesema baada ya kuchaguliwa ndani ya siku tisini ataanzisha utaratibu huo wa kuwapatia wazee bima ya afya kwani jambo hilo linawezekana na lipo ndani ya uwezo wake.
"Nitahakikisha ninatoa bima ya afya kwa kiwango cha mtumishi wa serikali kwa mwaka mzima ambapo wazee kuanzia miaka sitini na kuendelea watapata matibabu kwenye hospitali binafsi na za serikali" Alisema Mtweve.
Aidha Mtweve alisema barabara inayopita katika kata ya Isapilo ambayo imekuwa ikisumbua kwa muda mrefu na kushindwa kupitika wakati wa masika nayo itafanyiwa ukarabati ili iweze kupitika na wananchi wa kata hiyo.
"Tutajenga lami hata kama ni ya muda kwani lengo letu barabara ya Isapulano iweze kupitika muda wote ndani ya mwaka iwe kiangazi au masika" Alisema Mtweve.
Nae mgombea wa udiwani wa kata hiyo kupitia Chadema Fatma Ramadhani alisema miongoni mwa mambo ambayo atashughulikia kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama hicho pindi atakapochaguliwa ni wajasiriamali kushindwa kufanya biashara zao kutokana na kukosa fedha za kulipia kitambulisho cha Mjasiriamali.
"Ukiangalia mwananchi anapokosa fedha anatamani kubeba hata debe moja la mahindi ili akauze sokoni lakini anashindwa kuingia ndani kwasababu ya kukosa kitambulisho cha ujasiriamali" Alisema Fatma.
Post A Comment: