Mgombea wa Ubunge Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile (mwenye miwani) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi (mwenye kitambaa cheusi), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi (kushoto) kwenye kampeni za mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli leo wilayani Bahi.
Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake (CCM) Mariam Ditopile akiondoka kwenye mkutano wa kampeni za mgombea Urais wa chama hicho wilayani Bahi leo.
Charles James, Michuzi TV
MITANO tena! Ni kauli ya mgombea Ubunge wa Viti Maalum Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile aliyoitoa leo baada ya mgombea Urais wa chama hicho, Dk John Magufuli kufanya kampeni zake wilayani Bahi.
Akizungumza na Michuzi Blog, Ditopile ambaye alikua Mbunge wa Vijana katika Bunge lililopita amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Magufuli kwa miaka mitano ya awamu yake ya kwanza ni sababu tosha ya kumuongezea miaka mitano mingine.
Amesema ndani ya awamu yake ya kwanza Dk Magufuli amefanya kazi kubwa iliyovuka hadi matarajio na ahadi zake ambazo alizitoa mwaka 2015 alipokua akiomba kura kwa mara ya kwanza.
Mathalani kwenye eneo la uchumi, Ditopile amesema malengo ya Tanzania yalikua kufikia uchumi wa kati unaotokana na viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini Dk Magufuli amevuka lengo kwa kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati mwaka huu.
" Ni mambo ya ajabu na ya kipekee ambayo Dk Magufuli ameyafanya kwa kweli, fikiria miaka mitano tu katupeleka uchumi wa kati, pato la mtanzania mmoja mmoja limepanda kwa kasi kubwa, pato la Taifa limepaa, huyu mtu anastahili kupongezwa na pongezi pekee ni kumuongezea miaka mitano mingine.
Siyo kwenye uchumi tu kwenye usafirishaji Dk Magufuli ameturudishia Shirika letu la Ndege lililokua limekufa, ununuzi wa ndege 11 tena zinazotokana na fedha zetu wenyewe ni jambo la kumpongeza sana, niwaombe wana Dodoma na watanzania kwa ujumla Oktoba 28 twendeni tukamuongezee miaka mitano tena," Amesema Ditopile.
Akizungumzia sekya afya, Ditopile ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Wanawake amesema miaka mitano ya Rais Magufuli imekua yenye neema kwa wanawake nchini kwa sababu amejenga vituo vya afya zaidi ya 400 ambavyo vimeokoa maisha ya wakina mama wengi waliokua wakipoteza maisha wakati wa kujifungua.
Amesema ndani ya miaka minne hiyo Dk Magufuli amejenga Hospitali za Wilaya zipatazo 99 nchi nzima ambazo zimekua msaada kwa watanzania wengi hasa wanyonge.
" Ni sisi watanzania wanyonge ambao tulikua tunashindwa kupeleka watoto wetu shule kwa kukosa ada, lakini Dk Magufuli akasema hapana watoto wote kuanzia Shule ya Msingi hadi kidato cha nne atawalipia yeye ada, watanzania tunahitaji Rais wa aina gani zaidi ya Magufuli?" Amesema Ditopile.
Amesema wao kama wabunge wa Mkoa wa Dodoma wataendelea na kampeni kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo kutafuta kura za kishindo za mgombea Urais, wabunge na madiwani.
Post A Comment: