Na. Elinipa Lupembe.
Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amewataka wananchi wa halmashauri hiyo, kutambua kuwa kufanya usafi wa mazingira, katika maeneo yanayoyanayozunguka kwenye makazi na maeneo yao ya biashara ni jukumu lao na si jukumu la serikali.
Mkurugenzi Mtambule ameyasema hayo,baada ya kukerwa na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wafanya biashara, alipokuwa kwenye zoezi la siku maalumu ya usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi, lililofanyika eneo la Kwa Idd kata ya Olorien, Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni.
Amesema kuwa kila mwananchi anatakiwa kutambua kuwa, kufanya usafi wa mazingira ni jukumu lake na sio jukumu la serikali pamoja na kuhakikisha usafi unafanyika kwenye maeneo yote yanayowazunguka, na kuwa walinzi wa usafi katika maeneo hayo, kwa kumkamata mtu yoyote anayetupa taka ovyo.
Mtambule, amekemea na kupiga marufuku tabia ya watu hasa wafanya biashara wa chakula maarufu kama Mama Lishe ya kutupa mabaki ya vyakula, kumwaga majivu na kumwaga maji machafu nje ya maeneo yao ya biadhara, bila kujali usafi wa maeneo hayo na afya za wateja wanao wahudumia sambamba na majirani waliokaribu na biashara hizo.
"Kila mfanyabiadhara asafishe mazingira yanayomzunguka mpaka nusu ya barabara, lakini pia akusanye taka mpaka gari litakapokuja kubeba, na si kuyatupa kwenye mitaro, msikubali Mama Lishe watupe mabaki ya vyakula nje ya maduka yenu, toeni taarifa tutawatoza fani ya shilingi laki mbili na nusu " amesisitiza mkurugenzi huyo.
Ameongeza kuwa ni kosa kisheria kutupa takataka wala kumwaga maji machafu, nje ya maeneo yote yanayotuzunguka ikiwemo, maduka na barabara, hivyo simamieni usafi na kuwakamata watu watakaofanya uchafuzi huo, na watalipa faini.
Hata hivyo baadhi ya wafanya biashara wa maduka wamelalamikia tabia ya baadhi ya watu, wenye magari binafsi, kutembea na takataka kwenye mifuko, na kuzitelekeza pembezoni mwa barabara, ambapo ndio kwenye maduka yao, jambo ambalo linasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira maeneo ya barabarani.
Post A Comment: