Na.Faustine Galafoni,Dodoma.
Wahandisi kote nchini watakiwa kufanya kazi kwa ueledi,uzalendo na kwa kufuata maadili ya taaluma yao.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 3,2020 jijini Dodoma na katibu mkuu kiongoziBalozi Mhandisi John William Herbert Kijazi katika mkutano mkuu wa 17 wa bodi ya usajili wa wahandisi nchini ambapo amebainisha kuwa fani ya uhandisi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa ueledi kwa kuzingatia maadili na matakwa ya taaluma yao .
‘’Nitoe pongezi kwa wahandisi kwani mna mchango mkubwa ,muendelee kufanya kazi kwa uzalendo,na bodi ya usajili wa wakandarasi [ERB]iendelee kuwachukulia hatua wakandarasi wasiokuwa waaminifu,bodi bado mna jukumu kubwa kuhakikisha wakandarasi wasiokuwa waaminifu na wanaoenda kinyume na taaluma zao wanachukuliwa hatua”amesema.
Aidha,Balozi Kijazi amebainisha kuwa ni lazima wahandisi wawe wabunifu ,wadadisi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo hususan katika kipindi hiki cha mapinduzi ya nne ya viwanda.
“Tupo katika Mapinduzi ya 4 ya viwanda toka karne ya 18 hadi leo karne ya 21 ni lazima wahandisi wawe wabunifu ,mitaala ya vyuo lazima izingatie mapinduzi ya viwanda ,wahandisi ni vyema kushirikiana na taasisi zingine katika kufanikisha masuala ya teknolojia”amebainisha.
Katika hatua nyingine Balozi Mhandisi Kijazi ameainisha baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali ambapo mchango mkubwa unatokana na wahandisi ikiwa ni pamoja na Bwawa la Ufuaji wa umeme la Rufiji ,Mradi wa wa Reli ya Kisasa[SGR],upanuzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami huku pia akigusia ongezeko la ajira .
Katibu mkuu Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na mawasiliano Arch.Elius Mwakalinga amesema kuwa kwa kuwa maendeleo yanasimamiwa moja kwa moja na wahandisi ni vyema kulipa kipaumbele suala la wahandisi ambapo pia amebainisha kuwa Wizara inatumia gharama kubwa kuwasomesha wahandisi hivyo itahakikisha wahandisi wanabaki hapa nchini kulitumikia taifa huku akibainisha kuwa wahitimu 351 wa fani ya uhandisi wameshikizwa katika taasisi zilizo chini ya wizara na ametoa rai kwa taasisi zingine kuwaendeleza wahandisi.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa bodi ya usajili wa Wahandisi Tanzania[ERB]Mhandisi Prof.Ninatubu Lema amesema lengo la mkutano huo wa mwaka ni kubadilishana uwezo pamoja na kuwatambua wahandisi wapya waliohitimu ambapo pia amebainisha kuwa hadi sasa Tanzania ina jumla ya wahandisi 29,000 waliosajiliwa na bodi hiyo.
Aidha,Mhandisi Prof.Lema amesema Tanzania ina lengo la kufikisha wahandisi 80,000 ifikapo mwaka 2025 ambapo pia zaidi ya wahandisi 452 wameapishwa katika mkutano mkuu wa 17 wa wahandisi nchini.
Naye Msajili wa bodi ya Wahandisi Mhandisi Patrick Balozi amesema bodi hiyo imeanzisha chombo cha kuendeleza wahandisi huku akibainisha miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo kuwa ni pamoja na kusajili wahandisi,kuwaendeleza pamoja na kusimamia miiko ya wahandisi.
Kwa upande wake,Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge ametoa wito kwa vijana kuacha kuogopa kujaza fomu kwa ajili ya kusomea uhandisi kwani mahitaji yake ni makubwa huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwamo wahandisi kuwekeza viwanda ikiwemo uongezaji thamani katika zao la zabibu .
Akitoa salam kutoka ubalozi wa Norway,Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ms. Elisabeth Jacobsen akizungumza kwa njia ya video kupitia Mtandao wa ZOOM kwenye mkutano huo amesema serikali ya Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha sekta ya uhandisi inaendelea kukua huku akiipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendeleza mashirikiano hayo.
Jumla ya Mada 8 zinajadiliwa katika mkutano huo wa Wahandisi nchini ambapo pia washiriki kutoka nchini Norway,Botswana ,Uganda,Rwanda,na Kenya wamefuatilia mkutano wa 17 wa Wahandisi nchini Kwa video kupitia Mtandao wa Zoom na kutoa maoni yao ambapo mkutano huo unafanyika ukumbi wa mikutano wa Dodoma Convention Centre ukitarajiwa kuhitimishwa Septemba 4,2020.
MWISHO
Post A Comment: