TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, inawashikilia madereva watatu wa malori wakidaiwa kukwepa ushuru wa mazao .
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati Agosti 13 amesema madereva hao walishirikiana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kukwepa ushuru.
Anasema madereva hao walitumia magari aina ya malori yenye namba za usajili T450 AZP, KCM 411 L na KCU 073 X.
Amesema madereva hao walishirikiana na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo Peter Sanga na Joachim Soka kukwepa ushuru huo.
Amesema awali walipata taarifa ikiwatuhumu watumishi wa Halmashauri hiyo Sanga na Soka kwa kuhusika na kuhujumu mapato ya halmashauri kwa kutoa risiti za POS zinazoonyesha idadi ambayo ni nusu ya magunia ya vitunguu yanayokuwa yanasafirishwa na malori.
"Hivyo fedha za ushuru wa mazao ya magunia yanayozidi kwenye magari huingia mifukoni mwao badala ya kufikishwa sehemu husika," amesema Makungu.
Amesema kutokana na taarifa hiyo TAKUKURU kwa kushirikiana na polisi waliweka mtego uliowezeshwa kukamatwa kwa malori matatu yakiwa na shehena kubwa ya magunia ya vitunguu.
Amesema stakabadhi za mashine ya EFD zilionyesha kuwa wamelipia serikalini ushuru kidogo ukilinganisha na magunia ya vitunguu yaliyomo kwenye malori hayo.
Amesema watuhumiwa hao ambao ni madereva wa malori na mtumishi wa halmashauri hiyo Soka wanashikiliwa na TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi wa makosa ya kula njama na kuisababishia hasara halmashauri ya wilaya.
"Jaji mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma aliwahi kusema wakati akifungua kongamano la wadau wa mapambano dhidi ya rushwa katika mapambano dhidi ya rushwa katika mfumo wa utoaji haki Juni 17 mwaka huu kuwa utashi wa kisiasa na dhamira anayoonyesha Rais Magufuli hsitoshi bila ya kila taasisi, kila idara na kila halmashauri kukubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya rushwa," amesema Makungu.
Amesema taarifa za kufikishwa kwao mahakamani hupelekwa kwa uongozi wa Halmashauri hiyo ambapo tofauti na Halmashauri nyingine za mkoa huo huwasimamisha kazi mara moja kwenye halmashauri hiyo wanaendelea na kazi.
"Kwa msingi huo ni vigumu kupambana na rushwa ndani ya Halmashauri hiyo hadi pale viongozi watakapokubali kwa vitendo kwa vitendo kuwa sehemu ya kupambana na rushwa kuwasimamisha kazi.
"Ni rai yetu kwa viongozi wa Halmashauri hiyo wakaunga mkono utashi wa kisiasa na dhamira abayoonyesha Rais John Magufuli katika kupambana na rushwa ili kubadilisha mitazamo ya baadhi ya watumishi wanaona hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na mwajiri dhidi yao hata wanapofikishwa mahakamani kwa rushwa," amesema Makungu.
Post A Comment: