Na Allan Isack, ARUSHA

 MKURUGENZI  wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini(NEC), Dk.Wilson Mahera, amewataka waratibu wa Mikoa,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa Mikoa ya Arusha na Manyara kuhakikisha wanazingatia kanuni,sheria na maelekezo ya tume wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Hayo yalisemwa Jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya mpiga kura kutoka Tume ya  Taifa ya Uchaguzi, Dk.Cosmas Mwaisobwa, wakati akisoma hotuba ya Mkurugenzi wa NEC, Dk. Mahera Mahera, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa waratibu wa Mikoa,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

Mwaisobwa alisema, mafunzo hayo, yameshirikisha washiriki 116, kutoka  Mikoa ya Arusha na Manyara kwa lengo la kuwajengea uwezo wasimamizi hao, kusimamia mchakato wa uchaguzi  kuwa huru na wa haki kwa kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni na taratibu.

Hotuba hiyo, ilisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa na kuzingatiwa kwa kuwa hatua hizo, ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi.

Hata hivyo, alisema endapo sheria za uchaguzi,kanuni na utaratibu utazingatiwa  kutapunguza na kuondoa malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.


Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo, kuhakikisha siku tatu za mafunzo hayo, wanabadilishana udhoefu,kujadili namna ya kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, sambamba na kufikiria njia mbadala za kukabiliana na matatizo mbalimbali yatakayojitokeza wakati wa mchakato wa uchaguzi.


Hotuba ya Mkurugenzi huyo, ilisema kuwa pamoja na  baadhi ya washiriki kuwa na udhoefu wa kusimamia uchaguzi, aliwataka kuzingatia maelekezo watakayotolewa na tume badala ya kufanya kazi hiyo kwa mazoea.


“Tunaomba washiriki walioteuliwa kusimamia mchakato wa uchaguzi  waaminiwe, lakini wasifanye kazi hii kwa mazoea au uwezo wao binafsi, bali wafanye kwa kujiamini, kujitambua na kwa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi, kanuni,taratibu na maadili ,” alisema.

Mbali ya hayo, wasimamizi hao walitakiwa kuyajua na kuyatambua vyema maeneo watakwayokwenda kufanyia kazi, ikiwemo kuitambua miundombinu ya kuwafikisha katika kata na vituo vya kupigia kura ili kurahishisha shughuli ya upigaji wa kura kuanza mapema na kumalizika katika kwa wakati. 


Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Dk. John Pima, ambaye  ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, alisema  lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo washiriki na  kuwakumbusha washiriki kufuata maadili ya kazi yao na kuzingatia viapo walivyoapa.


Pima alisema, endapo kila mshiriki atawajibika na kutii kiapo chake alichokula itasaidia kutunza siri za uchaguzi, hivyo kutaepusha baadhi ya matatizo wakati wa mchakato wa uchaguzi.


Mkurugenzi wa Halmshauri ya Longido Mkoani Arusha, Dk. Jumaa Mhina, alisema kuwa jimbo lake lina jiografia ngumu ya kufika kutoka eneo moja kwenda lingine, lakini alisema amejipanga kikamilifu kukabiliana na tatizo hilo,  siku ya upigaji kura na vifaa vyote vitafika kwa wakati siku moja kabla ya upigaji kura .

Share To:

Post A Comment: