Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuyafanya mashindano maalum ya Paredi ya Mifugo yanayofanyika kila mwaka kwenye kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma kuwa Maonesho ya Kimataifa ya utalii wa mifugo ili kuongeza pato la taifa na kuleta hamasa kwa wananchi kushiriki.
Katika hotuba iliyotolewa kwenye Paredi la Mifugo leo na Mkuu ya Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Athuman Mukunda kwa niaba ya Wakuu hao wa Mikoa, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika hiyo uanzishaji uboreshaji wa Paredi la mifugo utasaidia kuinua uchumi wa taifa kwa kuongeza kipato kutoka kwa watalii kupitia mifugo.
Ameongeza kuwa jiografia ya Dodoma kuwa katika ya nchi na hali ya hewa nzuri ya majira ya mwezi Agosti katika eneo la Nzuguni linafanya watalii wengi kuja kutembelea maonesho hayo.
“Ndugu zangu niwaambie ukweli katika nchi yetu miongoni mwa Wizara mama ambazo ni nguzo na tegemeo wa maisha ya wananchi wake na ambayo inaweza kuongeza mapato ya Serikali ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi” alisisitiza Mhe. Mukunda
Amesema mifugo na uvuvi ni dhahabu inayotembea ambayo kama itatunzwa kwa kuzingatia ushauri na utaalam utaongeza tija na kulifanya taifa lisonge mbele kiuchumi
Hata hivyo amesema changamoto inayosababisha kutokuwa na mageuzi ya haraka kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini ni kukosekana kwa wataalam kwenye ngazi za chini kwa wananchi ambapo amesisitiza kuwa kuna umuhimu Wizara husika kushusha wataalam hadi kwenye ngazi za vijiji badala yahali ilivyo sasa ambapo wataalam wapo kwenye ngazi za juu jambo ambalo linafanya utalaamu usiwafikie wananchi kama ilivyokusudiwa.
Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya Wizara husika kuboresha ushirikiano katika utekelezaji na utoaji wa maelekezo ambapo amesema kumekuwa na ushahidi kuwa sehemu ambazo wizara zimeshirikiana kikamilifu na Halmashauri husika kumekuwa na matokeo chanya.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi amepongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo ameelekeza Halmashauri za Mkoa wa Singida kutenga maeneo kwa ajili ya kulima malisho ya mifugo na ameishukuru Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ikungi kuanzisha shamba darasa bora la malisho ya mifugo ambalo ni la mfano hapa nchini.
“Ukiona Mheshimiwa, Rais Dkt. John Magufuli anawekeza kwenye miradi kama ule wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere Rufiji, Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupola ya Singida lengo ni kujenga uchumi jumuishi” ameongeza Dkt. Lutambi
Amesema Mkoa wa Singida umendelea kupiga hatua katika kutekeleza miradi mbalimbali ambapo amesema licha ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye zao la Korosho pia wamesimamia vizuri sekta nyingine kama vile sekta ya madini ambapo muelekeo wa sekta ya madini ni kuwafanya wananchi wamiliki raslimali hii kwa kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amesema Serikali ya awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo ambapo viwanda vingi vya nyama vimeanzishwa, kuboresha kwa miundombinu ya mifugo kama majosho na kuimarisha minada, kuzuia utoroshaji wa mifugo kwenda nchi jirani na kuanza kutengeneza chanjo za mifugo ambapo hadi sasa chanjo sita zimekamilika na nyingine saba zinatarajia kukamilika katika kipindi kifupi kijacho na kufanya chanjo dhidi ya magonjwa 13 za kipaombele kukamilika.
Aidha, amesema Wizara ya Mifugo tayari imeshatangaza rasmi tarehe 13/5/2020 bei elekezi za chanjo za wanyama dhidi ya magonjwa 13 ya kipaombele kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 za Mwaka 2020 kifungu cha 3(2)(g) na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji Na 180 za Mwaka 2020 Kifungu cha 14(b) na (c) ambapo bei ya dukani nay a kuchanjia kwa dozi haitazidi viwango vilivyoainishwa.
Post A Comment: