Na Tito Mselem Shinyanga,
Waziri wa Madini Doto Biteko amesikitishwa na kitendo kilichotaka kufanywa na Uongozi wa Mgodi wa Madini ya Almasi wa Williamson Diamond Limited (WDL), uliopo Mwadui Wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga cha kutaka kuuza Mgodi huo kinyemela bila kuitaarifu Serikali.
Hayo ameyasemwa leo Julai 5, 2020 na Waziri Biteko alipofanya ziara kwenye mgodi huo baada ya kuona matangazo ya kuuzwa kwa mgodi huo kwenye mitandao ya kijamii.
Waziri Biteko amesema Serikali ina ubia wa asilimia 25 katika mgodi wa WDL, hivyo, haiwezekani utake kuuzwa bila mbia wake kufahamu na kueleza kuwa, kitendo hicho ni kukiuka taratbu na Sheria za nchi.
“Serikali ina ubia wa asilimia 25 kwenye mgodi huu kama mnataka kuuza mgodi lazima mtoe taarifa serikalini na mpate kibali, kwa mantiki hiyo serikali inapaswa kuwaadhibu kwa kutaka kuuza mgodi bila kibali huko ni kuhujumu nchi. Hvi mlituuliza serikali hatuna uwezo wa kununua mgodi na kuuendesha?,” amesisitiza Waziri Biteko.
Kutokana na kitendo hicho, Waziri Biteko ameuagiza uongozi wa mgodi huo ifikapo Julai 10 mwaka huu uwe umetoa maelezo kwa maandishi kueleza sababu za kutaka kuuza mgodi huo bila mbia wake ambaye ni Serikali kujua na pia kutoa taarifa ya kuwapunguza kazi wafanyakazi kisha kuwalipa nusu mshahara.
Amesema utaratibu uliotumika kupunguza wafanyakazi kwa kutumia kigezo cha ugonjwa wa Corona haufai na Wizara ya Madini hawakubaliani nao kutokana na pia wafanyakazi kulipwa mishahara nusu jambo ambalo linatoa wakati mgumu na kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, Waziri Biteko, amesema sababu ambazo zinatolewa na mgodi huo za kusitisha shughuli za uzalishaji na kutaka kuuza mgodi huo pamoja na kushuka kwa bei ya almasi duniani iliyosababishwa na ugonjwa wa corona, amezieleza kuwa hazina mashiko na kampuni husika inatakiwa kueleza ukweli na kama imefilisika ijulikane.
Waziri Biteko amesema sababu kubwa ambayo ingefanya mgodi huo kufungwa ni kushuka kwa uzalishaji na siyo uendeshaji, huku akihoji kama mgodi hauna fedha za kujiendesha ungetoa taarifa badala ya kuweka matangazo kwenye mitandao kuhusu kuuzwa mgodi wakati serikali haina taarifa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi huo Mhandisi Ayoub Mwenda, amekiri kuwa hawakutoa taarifa Serikalini juu ya kutaka kuuzwa kwa mgodi huo, huku akieleza kuwa walifunga mgodi huo April 8 mwaka huu kutokana na kushindwa kujiendesha na ameahidi kufuata maelekezo yote ambayo yametolewa na Waziri wa Madini.
Mhandisi Mwenda amesema Mgodi ilikuwa unazalisha vizuri kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona ambapo kwa mchanga Iliyokuwa umezalishwa waliokuwa walikuwa mbele kwa asilimia tatu na almasi zilizokuwa zimekusanywa walikuwa mbele kwa asilimia 9.1kulingana na bajeti yao Iliyokuwa imewekwa
Amesema tatizo la Corona limeuathiri sana mgodi huo na kusimama kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na kushuka bei ya masoko ya nje ambapo kabla ya Corona bei ilikuwa dola 246 kwa karati moja ambapo Machi mwaka huu waliuza karati moja dola 135 ambayo ilikuwa haiwezi kutosheleza gharama za uzalishaji.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba ameipongeza Wizara ya Madini kwa kazi nzuri inazofanya ambazo zimeisaidia nchi kuingia katika uchumi wa kati.
Post A Comment: