Ijapokuwa watu ni muhimu sana kwa mafanikio yetu, lakini wanaweza kugeuka na kuwa mwiba mkubwa kwa mafanikio yetu. Watu ambao tulizani watatutia moyo kipindi kigumu ndio haohao wanatukatisha tamaa. Marafiki ambao tuliwaamini ndio hao wanatusaliti. Watu ambao tunazani watatuhamasisha kupiga hatua katika mafanikio yetu, ndio hao wanaturudisha nyuma.
Watu ni muhimu kwa mafanikio yetu, lakini pia inatakiwa kuwa makini sana ni watu wa namna gani wamekuzunguka. Kama usipokuwa makini na watu waliokuzunguka itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa.
Wafuato ni watu unaotakiwa kuwaepuka katika maisha yako kama kweli unataka kufanikiwa:
Wakatishaji tamaa.
Watu kama hawa ukiwashirikisha mipango zako, lazima wakukatishe tamaa. Watakwambia maneno kama ‘ wewe huwezi’, ‘wengine wameshindwa utakuwa wewe?’, ‘haiwezekani’, na mengine kama hayo. Wao siku zote ni kukatisha tamaa na wanataka kukuona unabaki hivyo ulivyo.
Ubaya wa hawa watu wanaweza kuwa ndugu zako wa karibu, wanaweza wakawa wazazi wako, mpenzi wako, au ndugu wengine wa karibu. Wanaweza wakawa wanakukatisha tamaa kwa sababu wanakupenda na wanakuhurumia na hawataki kukuona unaumia.
Waepuke watu hawa kama unaweza kwenye maisha yako. Kama ni watu wako wa karibu sana unaweza ukaanza kupunguza muda unaokaa nao au ukaacha kabisa kuwashirikisha ndoto zako. Lakini pia unaweza ukawafundisha kwa kuwaelimisha kuhusu ndoto yako kwa kuwapa mifano ya watu ambao wamefanikiwa. Kama ukishindwa kuwaelimisha basi kaa nao mbali kadiri unavyoweza na usiwashirikishe mipango yako.
Tafuta watu watakao kutia moyo na sio kukukatisha tamaa. Waweke pembeni watu wanaokukatisha tamaa kama kweli unataka kufanikiwa.
Walalamikaji na wanung’unikaji.
Hawa ni watu wanaolalamika na kunung’unika kila muda. Wanalalamika kwa kila kitu na kila mtu. Hakuna kitu chochote kizuri wanachokiona kwenye maisha yao. Ni watu ambao hawako tayari kuwajibika na maisha yao. Ni watu wanaoilalamikia serikali kwa kila kitu. Wanaiona serikali kama ndio inawajibika na maisha yao.
Waepuke watu hawa, ukiambatana nao muda si mrefu na wewe lazima utaanza kulalamika na kunung’unika. Na ukishaanza kulalamika na kunung’nuka utashindwa kuwajibika na maisha yako.
Watu hasi.
Hili pia ni kundi la kuepuka. Hawa wanafanana na walalamikaji. Watu wanao ona na kuwaza mambo hasi tu. Siku zote wao kila kitu ni hasi. Mawazo yao ni hasi. Wanayoyasema ni hasi. Kila kitu wanakiona kibaya, hakuna kizuri kwenye maisha yao.
Watu hawa wanatafuta habari mbaya. Wanapenda kusikia watu wanashindwa. Hawasikii habari nzuri kwenye maisha yao. Habari mbaya ndo wanazopenda.
Watu kama hawa wakiwa karibu yako watakufanya na wewe huwe hasi. Watakufanya uanze kuwaona watu wengine pia ni hasi. Kila kitu utakiona hasi. Hata mawazo yako yataanza kuwa hasi.
Tafuta watu chanya kwenye maisha yako. Watu ambao wako tayari kubadilisha hali hata kama ni hasi kuwa chanya. Watu ambao hata kama wanaona udhaifu wako wanakwambia kwamba inawezekana. Ambatana na watu chanya kwenye maisha yako, watakuamasisha kufikia ndoto yako.
Wavivu na wapenda starehe.
Hawa ni watu wengine wakuwaweka pembeni kwenye maisha yako kama kweli unataka kufanikiwa. Watu ambao hawataki kufanya kazi kwa bidii. Watu wanaotaka mafanikio kwa njia rahisi. Watu ambao hawataki kujitoa kwenye kile wanachofanya.
Lakini pia watu wanaopenda starehe ni wa kuwaepuka. Watu wanaotanguliza starehe mbele na hawataki kufanya kazi. Sisemi kwamba starehe ni mbaya, kuna muda kweli unahitaji upumzike. Lakini starehe ikizidi inakuwa mbaya.
Waepuke hawa watu kama kweli unataka kufanikiwa.
Waongo na wasio waaminifu.
Uongo ni mbaya kwenye mafanikio yako. Watu wako wa karibu wakiwa waongo ni hatari sana kwa mafanikio yako.Uongo matokeo yake unaweza usiyaone kwa muda mfupi.
Ingawa Dunia ya sasa watu wakweli na waaminifu ni wachache lakini wapo, watafute na uambatane nao kwenye mafaniko yako. Unahitaji watu wakweli na watu wa kuwaamini katika safari yako ya mafanikio. Mtu ambae ukimpa kitu kufanya anakifanya kwa uaminifu. Unahitaji watu ambao wako tayari kukwambia ukweli hata kama unaumiza na sio watu wa kukwambia uongo ili ucheke.
Post A Comment: