Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dk. Fortunus Kapinga (kushoto) akizungumza na wakuu wa idara mbalimbali wa kituo hicho mwishoni mwa wiki, wakati walipokuwa wakikagua mashamba ya mfano yaliopo Viwanja vya Maonesho Nanenane Ngongo mkoani Lindi ikiwa ni maandalizi ya maonesho hayo ya Kanda ya Kusini yatakayoanza Agosti 1, 2020.

Shamba la mfano la migomba katika maonesho hayo. 
 Shamba la mfano la mtama katika maonesho hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dk. Fortunus Kapinga, akionesha bibo alilochuma  katika Shamba la mfano la korosho katika maonesho hayo.

  Shamba la mfano la mahindi katika maonesho hayo.
Shamba la mfano la mihogo katika maonesho hayo.
Shamba la mfano la ufuta katika maonesho hayo.
Bustani ya mchicha ya  mfano katika maonesho hayo.

Shamba la mfano la mikorosho katika maonesho hayo.
Mratibu zao la Korosho Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele, Dk. Geradina Mzena akizungumzia zao hilo.
Mtafiti Msaidizi, Betram Barnabas akizungumzia aina za magonjwa ya zao la korosho na namna ya kukabiliana nayo.
Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mawasiliano akizungumzia maandalizi ya maonesho hayo na kauli mbiu yake.
Afisa Kilimo, Samwel Tuluway akizungumzia kilimo cha bustani za mbogamboga mbalimbali katika maonesho hayo.
Mtafiti Mazao ya Nafaka na Mbegu, Juma Mfaume, akizungumza.
Mtafiti wa Mbegu za Mafuta, Athanas  Joseph, akizungumza.
Mtafiti Mkuu Kilimo (PARO), Bernadetha Kimata, akizungumzia kilimo cha mazao ya mizizi.
Mtafiti wa Zao la Viazi, Festo Masisila, akizungumzia kilimo cha zao hilo na faida zake.

Picha ya pamoja.




Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Mtwara.

KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo  mkoani Mtwara kinatarajia kuonesha teknolojia za kilimo za kuvutia katika Maonesho ya Nanenane 2020 Kanda ya Kusini yatakayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusu maandalizi ya maonesho hayo Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga alisema mwaka huu wamejipanga vilivyo kuonesha teknolojia zote za kilimo na litakuwa ni tukio la aina yake kwani kwa wale waliozoea kufika kwenye siku za nanenane sasa wataona shughuli endelevu za kituo hicho na kuwa wamefanya maboresho lukuki ya kisayansi  katika kila idara.

" Kituo cha Ngongo sio kwa ajili ya Nanenane tu bali kipo kwa mwaka mzima kueneza teknolojia  za kilimo na wataweza kuangalia teknolojia mbalimbali za korosho, mbegu za mafuta, mikungu, jamii ya mikunde na nafaka. Mbali ya hayo pia kutakuwa na shughuli ya kuangalia jinsi ya kuongeza thamani ya zao la korosho, ufuta na zao la karanga ambapo katika zao la korosho watu walizoea kuja na kutafuna korosho lakini sasa watakuja kula na kunywa korosho kwani watakuwa na juisi, jamu na mvinyo zilizotokana na zao hilo" alisema Kapinga.

Alisema TARI Naliendele ina majukumu ya kufanya utafiti wa mazao makubwa kitaifa ya korosho na mbegu za mafuta ambayo ndani yake kuna ufuta na karanga.

Alisema katika maonesho hayo watakuwa na kituo chao cha kanda na wamejipanga kuonesha teknolojia za kilimo kwa mwaka mzima na sio kama walivyozoea hivyo wadau mbalimbali wameombwa wafike kwani wataona mengi kwenye zao la korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi, uwele na mengineyo.

Alisema mazao yote ambayo yanalimwa kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi na hata yale ambayo hayalimwi katika mikoa hiyo lakini yanaweza kustawi maeneo hayo yatakuwepo katika maonesho hayo.

Kapinga alisema katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu pale wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu,  shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.

" Tukisema mkulima au mdau aje wakati wa wiki ya Nanenane tu kuna hatua nyingi hawezi kuzielewa na ndio maana tunasema hatufungi maonesho haya tupo kipindi chote cha mwaka mzima." alisema Kapinga.

Alisema TARI imekuwa ikisogeza huduma zake kwa wananchi nchi nzima ili ziwafikie walengwa.

Alisema zamani zao la korosho lilikuwa likilimwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani lakini sasa linalimwa karibu mikoa zaidi ya 20 kama Morogoro, Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Katavi, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe,  Mkoa wa Kilimanjaro  maeneo ya Same.

Alisema kinachosemwa korosho ilimwe wapi sio mipaka ya kiutawala bali ni mahitaji ya kiikolojia.

Kapinga alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima na wadau mbalimbali kufika kwenye maonesho hayo ya Kanda ya Kusini yatakayofanyika Ngongo mkoani Lindi kuanzia Agosti 1,2020 kwenda kujifunza teknolojia za kilimo.

Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mawasiliano alisema jukumu lake kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.

"TARI Naliendele tunafanya utafiti na ukishafanywa kazi yetu ni kutoa matokeo ya utafiti huo na idara yangu kazi yake kubwa ni kuuchambua na kuchakata taarifa za utafiti huo na kuziweka katika lugha nyepesi ambayo inaweza kuwa rahisi kwa wakulima na wadau wengine kuielewa" alisema Kidunda.

Kidunda alisema kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora mwaka 2020.


Share To:

Post A Comment: